Sakata la mwanamke anayelalamikia kubadilishiwa mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru limechukua sura mpya baada ya Wizara ya Afya kuingilia kati na kuagiza uchunguzi wa vinasaba (DNA).
Neema Kilugala, mkazi wa Daraja Mbili, Arusha, alijifungua kwa njia ya upasuaji tarehe 24 Machi 2025 katika hospitali hiyo. Anadai kuwa baada ya kujifungua alioneshwa mtoto wake akiwa mzima, lakini baadaye aliletewa mtoto aliyekuwa amefungwa vitenge visivyo vyake.
"Nilipohoji, muuguzi aliniambia kuwa alichanganya vitenge na vya mtoto mwingine na akaahidi kurekebisha hali hiyo. Lakini bado nilikuwa na wasiwasi kama kweli huyu ndiye mwanangu," alisema Neema.
Malalamiko yake yamesambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii, yakiibua mjadala mpana kuhusu usalama wa watoto wachanga hospitalini.
Kufuatia hali hiyo, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha pamoja na Jeshi la Polisi imechukua hatua zifuatazo:
-
Kuagiza uchunguzi wa vinasaba (DNA) wa wazazi wote waliyojifungua katika kipindi hicho pamoja na watoto wao ili kubaini ukweli.
-
Kumsimamisha kazi muuguzi aliyehusika ili kupisha uchunguzi.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Roida Andusamile, amesema kuwa hatua hizi ni muhimu kuhakikisha haki inatendeka.
"Tunasubiri matokeo ya uchunguzi wa DNA kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali. Baada ya uchunguzi kukamilika, taarifa rasmi zitatolewa na hatua stahiki zitachukuliwa," alisema Roida.
Kwa sasa, familia ya Neema inaendelea kusubiri matokeo ya uchunguzi huo huku ikitaka haki ifanyike.
Tukio hili limezua taharuki kubwa na kuibua maswali kuhusu uwajibikaji wa wahudumu wa afya na ulinzi wa watoto wachanga hospitalini.
0 Comments:
Post a Comment