Watumishi wa Umma Wachochea Migogoro Kushughulikiwa: Timu ya Samia Legal Aid Yapiga Kambi Arusha

 


Timu ya watoa huduma wa msaada wa Kisheria kupitia kampeni ya "Samia Legal Aid Campaign" imeagizwa kuorodhesha majina ya watumishi wa serikali katika sekta mbalimbali watakaobainika kutajwa na wananchi kuwa wanachochea migogoro inayopelekea wananchi kuichukia Serikali.



Maagizo hayo yametolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Christian Makonda, wakati akiongea na wataalam wa sheria wakiwemo mawakili, maofisa maendeleo ya jamii pamoja na wakuu wa idara na vitengo mbalimbali waliokutana kwa ajili ya kupanga mikakati ya utatuzi wa changamoto za wananchi katika halmashauri saba za Mkoa wa Arusha pamoja na kuainisha changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi katika kila idara husika.


Makonda alisema, "Kuna baadhi ya maofisa maendeleo ya jamii wanalalamikiwa kwa kupindisha sheria ikiwemo watumishi wengine hivyo katika kampeni hiyo endapo kuna watumishi wanalalamikiwa kukwamisha utatuzi wa migogoro kwa wananchi wakuu wa timu husika kutoka Wizara ya Katiba na Sheria waandike majina yao kisha mwisho wa kampeni hiyo watoe taarifa kwake ili hatua stahiki zichukuliwe."



Aidha, alisisitiza kuwa, "Kuna baadhi ya watumishi wanatajwa na wananchi kutokana na tabia ya kukwamisha mambo tunaomba majina yao, lakini pia naomba timu hizi zianishe changamoto zote zilizoibuka ili kupelekwa mahali husika kama polisi, uhamiaji, idara ya kazi na kwingineko ili hatua stahiki zichukuliwe."



Vilevile, Mkuu huyo wa Mkoa aliwasihi watoa huduma kuhakikisha wanawasilikiliza wananchi wanaofika kwa msaada, akisema, "naomba timu hizi zianishe changamoto zote zilizoibuka ili kupelekwa mahali husika kama polisi, uhamiaji, idara ya kazi na kwingineko ili hatua stahiki zichukuliwe." 


Aliongeza kuwa ni muhimu kwa watoa huduma hawa kujiuliza "nafsini kwao je maamuzi watakayotoa ni sahihi na hakuna upendeleo ili wahusika wapate haki yao kwa mujibu wa changamoto zao."



Kwa upande mwingine, Ester Msambazi, ambaye ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, alieleza kuwa kampeni hii ilianza kutekelezwa mwaka 2023 na Mkoa wa Arusha ni wa 23 tangu kampeni hii kuanza. 





Aliongeza kuwa wamejipanga vizuri kuanza kutoa msaada huu kwa wananchi, akisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha haki inapatikana kwa urahisi.


Uzinduzi wa kampeni hiyo utafanyika Machi 28, 2025 kwenye viwanja vya Ngarenaro, ambapo Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, pamoja na  Makonda watahudhuria. 


Katika uzinduzi huo, huduma na elimu za kisheria zitolewe, ikiwa ni pamoja na huduma kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Polisi, na idara na ofisi mbalimbali za serikali ambazo zitatoa huduma za bure kwa wananchi. Baada ya uzinduzi, timu husika zitakwenda uwandani kuanza kazi rasmi Machi 29, mwaka huu.


Kampeni hii ni muhimu kwa kuhakikisha haki inatolewa kwa wananchi bila vikwazo, na inaonekana kuwa ni hatua muhimu katika kudhibiti tabia za baadhi ya watumishi wa serikali wanaochochea migogoro au kukwamisha haki.


0 Comments:

Post a Comment