Papa Francis Aondoka Hospitalini, Aelekea Nyumbani kwa Mapumziko ya Miezi Miwili

 




Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, ameondoka hospitalini baada ya kuwa huko kwa zaidi ya mwezi mmoja, akipatiwa matibabu kutokana na changamoto za kiafya. 


Kwa mujibu wa madaktari waliokuwa wakimtibu katika Hospitali ya Gemeli, mjini Roma, Papa anatarajiwa kuondoka hospitalini baadaye leo na kurejea katika makazi yake rasmi huko Vatican, ambapo atakuwa chini ya uangalizi wa karibu kwa muda wa miezi miwili.


Papa Francis, ambaye alilazwa hospitalini mnamo Februari 14 akiwa na changamoto za mfumo wa kupumua na nimonia, ameendelea kupata matibabu kwa wiki tano. 


Katika kipindi hiki, alikumbwa na changamoto zaidi za kiafya, na madaktari wamesema kwamba maisha yake yalikuwa hatarini. 


Hata hivyo, daktari wake, Sergio Alfieri, ameonyesha furaha kwamba Papa sasa atarejea nyumbani, ingawa atahitaji muda mrefu kwa sauti yake kurejea kwenye hali ya kawaida kutokana na matibabu ya oksijeni aliyopokea.

Katika hatua ya kipekee, Papa anatarajiwa kuonekana hadharani kwa mara ya kwanza baada ya kuondoka hospitalini, saa nane za jioni saa za Afrika Mashariki (saa sita mchana za Roma). 


Atakuwa akibariki waumini waliokusanyika nje ya hospitali hiyo kumuombea apate afueni, kisha ataondoka kuelekea kwenye makazi yake rasmi huko Vatican.

Madaktari wamesema kuwa, kutokana na hali ya kiafya ya Papa, hatoweza kutangamana na watu wengi kwa kipindi cha miezi miwili hadi atakapohakikishwa kuwa afya yake imetengemaa kabisa. Hali hii inahusiana na changamoto alizokumbana nazo baada ya kupata matibabu ya oksijeni, ambayo yanaweza kudhoofisha koo na kuathiri uwezo wa kuzungumza, jambo ambalo litachukua muda kufufuka.

Wengi wanategemea kwamba Papa atakuwa na afya bora ndani ya miezi miwili, ingawa haijulikani kwa sasa kama atahudhuria au kuongoza ibada ya Pasaka, kama ilivyokuwa desturi yake kila mwaka.

Katika kipindi hiki cha mapumziko, Papa Francis anatarajiwa kuwa chini ya uangalizi wa madaktari na wataalamu wa afya ili kuhakikisha anapata nafuu kamili.

0 Comments:

Post a Comment