
Wakati Vyama 18 vya siasa vyenye usajili kamili, Serikali na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi wamesaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2025, chama kikuu cha upinzani nchini, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hakikusaini kanuni hizo, hivyo kujiondoa rasmi kwenye uchaguzi mkuu wa 2025 na chaguzi ndogo zitakazojitokeza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Vyama vilivyosaini ni pamoja na Chama cha Mapinduzi (CCM), Civic United Front (CUF), NCCR-Mageuzi, UMD, NLD, UPDP, NRA, ADA-TADEA, TLP, UDP, MAKINI, DP, SAU, AAFP, CCK, ADC, CHAUMMA na ACT-Wazalendo.
Kwa upande wa Serikali, Kanuni hizo zilisainiwa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi, na kwa upande wa Tume zilisainiwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele.
"Tunawashukuru viongozi wote wa Vyama vya Siasa kwa namna ambavyo mmekuwa mkiipa ushirikiano Tume katika utekelezaji wa majukumu yake mbalimbali hususan yale yanayohusu mchakato wa maandalizi ya uchaguzi, ikiwemo uandaaji wa Kanuni za Maadili ya Uchaguzi ambazo tupo hapa leo kwa ajili ya kutia saini kwa ajili ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2025," alisema Jaji Mwambegele.
Alifafanua kuwa Kanuni hizo zimeandaliwa kwa mujibu wa kifungu cha 162 cha Sheria ya Uchaguzi Na. 1 ya Mwaka 2024, na kwamba vyama vya siasa pamoja na Serikali walipata fursa ya kutoa maoni yao kuanzia tarehe 1 hadi 14 Machi, 2025.
"Napenda kutoa shukrani za dhati kwenu kwa ushiriki wenu katika kuandaa rasimu hiyo kwa kutoa maoni yenu na kuyawasilisha Tume kwa wakati," aliongeza Jaji Mwambegele.
Kwa upande wa Tume, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima R. K, alisema:
"Vyama vya siasa vina wajibu wa kufanya kampeni za kistaarabu na kujiepusha na mambo yanayoweza kupelekea uvunjifu wa amani."
Alisisitiza kuwa:
"Chama ambacho hakijasaini maadili hayo hakitopata fursa ya kushiriki kwenye uchaguzi mkuu na chaguzi ndogo nyingine zote zitakazofanyika kwa kipindi cha miaka mitano ijayo."
Aidha, alibainisha kuwa Serikali ina wajibu wa kutoa fursa sawa kwa vyama vya siasa kutumia vyombo vya habari vya umma na kuhakikisha hali ya amani na utulivu inatawala kipindi chote cha uchaguzi.
Wakati hayo yakiendelea jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, alitangaza msimamo wa chama hicho kupitia mtandao wa X (zamani Twitter), akisema:
"Katibu Mkuu @ChademaTz sitakuwepo kwenye kikao cha tarehe 12 Aprili 2025 cha kushauriana na kusaini maadili ya uchaguzi ya 2025."
Ifahamike kuwa mwenye mamlaka ya kusaini maadili ya uchaguzi kwa niaba ya chama cha siasa ni Katibu Mkuu.
"Katibu Mkuu sijateua kiongozi au afisa yoyote kwenda kushiriki kwa niaba yangu katika kikao hicho kitakachofanyika katika Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi @TumeUchaguziTZ Mkoani Dodoma," ametangaza Mnyika kupitia mtandao wa X.
"Sitakwenda Dodoma kusaini wala sitatuma mwakilishi."
Alisisitiza msimamo wa chama hicho kwa kauli maarufu:
"No reforms, no election."
Msemaji wa Chadema, Brenda Rupia ametoa taarifa kwa umma akisema hatua hiyo ya kutosaini kanuni za maadili hii leo imetokana na kile alichodai kuwa ni kutokujibiwa kwa barua yao iliyotumwa Disemba 2024 kuhusu "mapendekezo na madai ya msingi ya Chadema kuhusu mabadiliko ya mfumo wa
Anasema ukimya wa tume "unathibitisha kukosekana kwa nia ya dhati ya kufanya mashauriano ya kweli na uwazi kuhusu mchakato wa uchaguzi.
Chadema tayari ipo katika kampeni ya 'No reforms, no election' ikimaanisha bila mabadiliko, hakuna uchaguzi. Kampeni hiyo ambayo imekuwa ikiongozwa na Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu inalenga 'kuzuia' uchaguzi kufanyika endapo matakwa ya chama hicho hayatatekelezwa.
Lissu alishtakiwa kwa uhaini juzi Alhamisi akituhumiwa kuchochea uasi. Mashtaka hayo yanatokana na moja ya kauli zake aliyoitoa kuhusu kuzuia uchaguzi.
Makamu mwenyekiti wa Chadema, John Heche ametangaza kuwa kampeni hiyo itaendelea licha ya mwenyeliti Lissu kuwa mahabusu.
Chadema inaamini bila mabadiliko ya kimfumo, uchaguzi wa Oktoba 2025 hautakuwa huru na wa haki, madai yanayopingwa vikali na chama tawala cha CCM pamoja na serikali.
Hatua ya CHADEMA kujiondoa kwenye mchakato huo inaashiria mwelekeo mpya wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, huku mjadala wa marekebisho ya sheria na mifumo ya uchaguzi ukiendelea kuwa kitovu cha mvutano kati ya vyama vya upinzani na mamlaka husika.
0 Comments:
Post a Comment