Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Arusha (RCC), kilichofanyika Desemba 18, 2024, katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, kimejadili kwa kina suala la ombaomba katika mkoa huo na kuweka mikakati ya kudhibiti hali hiyo. Aidha, kikao hicho kimepokea mapendekezo ya kufutwa kwa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Ngaramtoni, kufuatia malalamiko ya gharama kubwa za uendeshaji wake.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Suleiman Msumi, alieleza kuwa mapendekezo hayo yanatokana na malalamiko ya wananchi.
“Uamuzi huu unatokana na malalamiko ya wananchi ambao wamedai kuwa gharama za huduma za uendeshaji wa Mamlaka ya mji mdogo wa Ngaramtoni ni kubwa sana,” alisema.
Msumi alifafanua kuwa malalamiko hayo yaliwasilishwa kupitia mikutano ya hadhara iliyofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha, ambapo wananchi waliomba kufutwa kwa mamlaka hiyo.
Akizungumzia suala la ombaomba, Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Misaile Mussa, alieleza kuwa maeneo yanayotumiwa na walemavu hao si salama kwao.
“Kupitia timu ya wataalamu wa Mkoa, tutafuatilia kwa ukaribu suala hili bila kusababisha ukatili au kudhalilisha utu wao,” alisema
Mussa aliongeza kuwa Halmashauri ya Jiji la Arusha ina zaidi ya shilingi bilioni 6 kwa ajili ya mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana, na walemavu, akiwahimiza walemavu kuchangamkia fursa hiyo.
“Badala ya kukaa barabarani kuhatarisha maisha yao, waombe mikopo hiyo ili waweze kufanya biashara zitakazowapatia kipato,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Dadi Kolimba, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, alisema maafisa ustawi wa jamii na maafisa maendeleo ya jamii wamepewa jukumu la kuwafuatilia walemavu hao ili kujua wanakotoka.
“Tumekubaliana kutumia viongozi wa mitaa, ambao wanawafahamu vyema wakazi wa maeneo yao, ili kuwabaini walemavu wanaotoka nje ya mkoa,” alisema Kolimba.
Pamoja na hayo, kikao hicho kimeazimia kila wilaya kutenga maeneo maalum kwa ajili ya uwekezaji na utalii, huku wajumbe wakisisitiza umuhimu wa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo na matumizi sahihi ya fedha za miradi hiyo.
Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, John Palangyo, alisifu maazimio ya kikao hicho akisema kuwa yatasaidia kuchochea maendeleo ya mkoa wa Arusha.
“Kupandisha hadhi ya maeneo na kufuta baadhi ya mamlaka kutasaidia ukuaji wa maendeleo na kuongeza mapato kwa halmashauri na mkoa kwa ujumla,” alisema.
Aidha, kikao hicho kiliazimia kufikisha ombi la kufuta Mamlaka ya Mji Mdogo wa Ngaramtoni kwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa hatua zaidi.
Wajumbe pia walipendekeza kuundwa kwa kamati ya mkoa itakayoshughulikia upandishaji wa hadhi ya halmashauri kuwa manispaa, ambapo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, John Maha, alisema: “Halmashauri zikipandishwa hadhi na kuwa manispaa zitachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya haraka.”
0 Comments:
Post a Comment