Ajali Yaua Saba, Wakiwemo Wanakwaya Sita wa KKKT, 75 Wajeruhiwa Same

 


Ajali mbili zilizotokea wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, zimelighubika eneo hilo kwa huzuni baada ya watu saba kupoteza maisha, wakiwemo wanakwaya sita wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), usharika wa Chome. 


Zaidi ya majeruhi 75 waliripotiwa, wakiwa na majeraha mbalimbali.


Ajali ya kwanza ilitokea majira ya saa saba usiku wa kuamkia leo katika eneo la Njoro, ambapo basi la Kampuni ya Osaka, lililokuwa likielekea Dar es Salaam, lilihusika. 



Ajali hii ilisababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi watu 52. Maelezo kutoka kwa baadhi ya majeruhi wanasema kuwa chanzo cha ajali hiyo kilikuwa ni mwendokasi wa dereva, hali iliyosababisha gari kushindwa kutawala.



Ajali ya pili, inayohusisha basi aina ya Costa la Kampuni ya Mkokota, ilitokea majira ya saa mbili asubuhi leo katika milima ya Ilamba. 



Basi hili lilipinduka baada ya kushindwa kupanda mlima, na kusababisha vifo vya watu sita, wakiwemo wanakwaya wa KKKT walikuwa wakielekea Ndolwa kueneza Injili kwa njia ya nyimbo. 



Chanzo cha ajali hii kimeelezwa kuwa ni hitilafu ya mfumo wa usukani wa gari (steering rod).



Mganga Mkuu wa Wilaya ya Same, Dkt. Alex Alexander, alithibitisha kupokea majeruhi 23 kutoka ajali ya pili, wakiwa na majeraha mbalimbali, baadhi wakiwa na mifupa iliyovunjika. 


Miili ya marehemu sita imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti ya hospitali ya Same, ikisubiri utambuzi wa familia zao.



Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, alielezea masikitiko yake kuhusu vifo hivyo na kuhimiza madereva kuwa makini wanapopita katika wilaya hiyo, hasa kutokana na hali ya hewa yenye upepo mkali. Alisisitiza pia umuhimu wa abiria kutoa taarifa kwa mamlaka husika endapo watabaini hali yoyote inayoweza kuhatarisha usalama wao, kama vile mwendokasi au hali ya barabara.

Ajali hizi zinatoa zitumike kuwakumbusha madereva, abiria, na mamlaka za usalama barabarani kuwa makini na kufuata sheria ili kuepusha majanga kama haya

0 Comments:

Post a Comment