Na Ezekiel Kamwaga
MARA nyingi ninapofanya uchambuzi kuhusu wanasiasa, huwa ninaamini kuwa kuna wanasiasa wa aina tatu; wanasiasa wa kipekee, wanasiasa wa kitaasisi na wanasiasa wa msimu.
Wanasiasa wa kipekee ni wale ambao si wa kawaida. Nazungumzia watu wa aina ya Nelson Mandela wa Afrika Kusini, Kwame Nkrumah wa Ghana, Julius Nyerere wa Tanzania na wengine wa aina hiyohiyo. Kwa sababu za kihistoria na za kimuktadha, nchi nyingi hazizalishi viongozi wengi wa aina hii.
Wanasiasa wataasisi ni wale ambao wao hujenga taasisi za kisiasa katika mazingira ambayo na wenyewe huwa ni taasisi. Hawa ni wanasiasa wa aina ya Raila Odinga, Seif Shariff Hamad, Abdoulaye Wade, Etienne Tshisekedi nikitumia wale wa upinzani.
Yoweri Museveni ni mwanasiasa mtaasisi. Paul Kagame wa Rwanda ni mwanasiasa mtaasisi. Na viongozi wengine kama vile Paul Biya, Omar Bongo na wengine. Wanaweza kuwa hawana karama kama za wa kundi la kwanza lakini wanajua namna ya kudumu kwenye siasa.
Halafu kuna kundi la tatu. Hili ni la wanasiasa ambao huibuka na kuwa maarufu kwa sababu ya nyakati fulani za kisiasa na kihistoria katika nyakati. Kama nyakati hizo zisingetokea, wasingekuwa na umaarufu au vyeo walivyonavyo.
Chukulia mfano wa Adama Barrow, Rais wa sasa wa Gambia. Kama isingekuwa kwa Rais Yahya Jammeh kuwafunga jela viongozi wote mashuhuri wa upinzani wa Gambia, yeye asingeweza kushika wadhifa huo.
Ilibidi ijitokeze fursa ya Jammeh kuchokwa, waliokuwa na ushawishi zaidi yake kuwa jela, ndipo naye bahati imwangukie. Miaka miwili nyuma au miezi mbele ya wakati ule, Barrow asingekuwa alipo.
Katika mchuano wa uchaguzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) uliopamba moto baada ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho mtawalia, Freeman Mbowe na Tundu Lissu, wote kuchukua fomu kuwania Uenyekiti, mawazo yangu moja kwa moja yakaenda kwa makundi yangu hayo ya wanasiasa.
Kwangu, Mbowe anaangukia katika kundi la mwanasiasa mtaasisi. Yeye ni mtu mmoja lakini katika chama chake yeye ni taasisi inayojitegemea kutokana na historia yake ndani ya chama hicho.
Lissu anaangukia katika kundi la tatu. Hili ni kundi la wanasiasa wa msimu. Namna pekee ya Lissu kushinda uchaguzi dhidi ya mtaasisi ni katika mazingira fulani ambayo kila nikiyatazama sasa – kwa kadri nitakavyoeleza baadaye, naona hayapo.
Wanasiasa wataasisi wana ngozi ngumu, wananyumbulika, ni wavumilivu na wanajua wakati wa kushambulia. Unyumbulifu wao ni silaha kubwa kwa sababu unawafanya waweze kuishi kwa muda mrefu na kwa namna tofauti.
Chukulia mfano wa Vladmir Putin wa Russia. Kuna wakati alikuwa tayari kuwa Naibu Rais wa Russia na kumwachia nafasi hiyo Dmitry Medvedev akijua baadaye atakuja kushika wadhifa huo.
Kwa sababu ya kile kilichotokea kwa chama cha ACT Wazalendo kwa aliyekuwa Kiongozi wa Chama (KC) kuachia ngazi, labda mtu angetafutwa kuzungumza na Mbowe kuhusu uwezekano wa CHADEMA kufanya kitu kama hicho lakini kutengeneza jukumu ambalo bado Mbowe angekuwa na ushawishi mkubwa kwenye chama lakini wakati huohuo kuonekana kwamba hajang’ang’ania madaraka. Ingetafutwa tu namna ya kumpa amani badala ya kuingia naye vitani.
Wanasiasa wataasisi wanajua kutunza mahusiano na watu – hata wale ambao hawawaamini kabisa, wanajua namna ya kuatamia mamlaka na wanajua umuhimu wa kuwa na silaha muhimu katika siasa – rasilimali zote muhimu – watu na fedha.
Wanasiasa wa msimu hawana uwezo wa kutunza marafiki wala kujua namna ya kuatamia mamlaka kwa sababu huwa hawako karibu na mamlaka namna hiyo. Na kwa sababu kwa muda mrefu wanakuwa hawana nia dhabiti ya kuwania nafasi ya juu kabisa, huwa hawana mtandao wa kutosha – wa marafiki na nusu marafiki, wa kuwasaidia kuvuka mstari wakati itakapohitajika.
Ndiyo sababu Raila Odinga amewania urais Kenya mara lukuki na kushindwa lakini kila mara anarejea tena. Huwezi kumpindua Raila kwa sababu ana rasilimali watu na fedha za kutosha kujua nini kinaendelea upande wa pili.
Haikuwa rahisi pia kumtoa Maalim Seif alipokuwa CUF wala ACT Wazalendo na Wade hakuondolewa na wenzake kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 1980 hadi hatimaye ‘kilipoeleweka’ mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Nimecheka wiki iliyopita wakati mtu mmoja alipoandika mitandaoni kwamba Mbowe anatakiwa kuachia ngazi kwa sababu ameshindwa vibaya kwenye uchaguzi wa mitaa. Nilicheka kwa sababu jambo moja linalowafanya wanasiasa wataasisi kudumu madarakani ni ile dhana kwamba huwa hawashindwi kihalali.
Mwandishi alikuwa anamaanisha kwamba Mbowe anatakiwa kuachia ngazi kwa sababu ya matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2020 na huu wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwezi uliopita. Swali ambalo hakutaka kujiuliza ni jepesi tu; Je, wafuasi wake wanaamini kwamba Mbowe alishindwa kihalali?
Washabiki kindakindaki wa Maalim Seif, walikuwa wanaamini kwamba alishindwa katika uchaguzi wa miaka ya 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015? Kama hawaamini hivyo, kuna hoja kuwataka waachie ngazi kwa sababu walishindwa uchaguzi?
Katika vita kati ya mwanasiasa mtaasisi na mwanasiasa wa msimu, mtaasisi atashinda saa nne asubuhi. Sishangai kwamba wengi wa wanaomuunga mkono Lissu, hasa mitandaoni, wanamwomba Mbowe aachie ngazi.
Tundu hakuwa na sababu ya kutoa makucha yake mbele ya Mbowe. Kama ilivyokuwa mwaka 2020 ambapo busara iliamua kuwa Lissu alikuwa anafaa kuwania urais kuliko Mbowe kutokana na mazingira ya wakati ule, kungeweza kutokea fursa ambapo ni Lissu pekee ndiye angekuwa mtu wa kuikamata. Hii ni kwa sababu, kwa sasa na kwa mazingira yaliyopo ndani ya chama hicho, Lissu hawezi kumshinda Mbowe kupitia sanduku la kura. Sijajua kwa nini mtu anaamua kuingia katika vita ambayo anajua hawezi kushinda.
Kihistoria, wanasiasa wataasisi wanaachia ngazi kwa sababu kubwa mbili tu; mosi suala linaloamuliwa na Mungu – kwa maana ya sababu za kiafya au kifo na pili ni kwa sababu ya kupewa dili ambayo hawezi kuikataa. Raila anaondoka kwenye siasa za Kenya kwa kupewa mchuzi wa kuongoza taasisi ya Umoja wa Afrika.
Kama mimi ningekuwa Lissu na nataka kuchukua nafasi ya Mbowe, ningetafuta jambo ambalo naweza kuliweka mezani na kiongozi huyo wa chama kwa takribani miaka 20 akaamua kuachia ngazi. Si lazima jambo hili litokee kwenye mazungumzo ya Lissu na Mbowe au na watu wao. Mbowe hajawahi kukataa kukaa mezani kujadili jambo na kama ingewekwa mezani dili – nikimaanisha, jambo ambalo angeweza kulifanya na kuwa mkubwa zaidi au manufaa zaidi, huenda angekubali.
Lakini kwa kuwa Lissu kaamua kuingia ulingoni, jambo moja linaweza kutokea. Ni kwamba Mbowe atatumia nguvu na ushawishi wake wote kuhakikisha Lissu haji tena kumsumbua kama ilivyotokea mara hii. Mara nyingi huwa hakuna mwisho mzuri kwa Makamu pale anapoonyesha kutaka kutanua misuli yake mbele ya Mwenyekiti ambaye ni mtaasisi. Wataasisi huwa hawaruhusu uwapo wa mafahari wawili ndani ya zizi moja.
Bahati mbaya kwa Lissu ni kwamba bila ya CHADEMA, ni mwanasiasa wa kawaida. Nguvu ya umma na rasilimali ya chama chake cha sasa ndiyo ilikuwa inampaisha na kumfanya kuwa jirani na madaraka.
Nje ya CHADEMA, kama Lissu ataenda chama chochote cha siasa au kuanzisha chake, hataweza kushindana na chama chake hiki cha sasa. Kimsingi, bila CHADEMA, Lissu hawezi kushindana na ACT Wazalendo ya Zitto Kabwe.
Anaweza kuwa na chama kama cha Democratic (DP) cha enzi za hayati Mchungaji Christophet Mtikila, ambapo kitajulikana na watu watafurahi kumsikiliza bila ya kwenda popote kisiasa.
Labda, labda, utokee msimu huko mbele ya safari ambako ni yeye pekee ndiye atakuwa amejaaliwa bahati ya kuushika.
Ezekiel Kamwaga ni Mwandishi wa Habari na Mchambuzi wa Masuala ya Siasa.
0 Comments:
Post a Comment