Uzinduzi wa Ripoti ya Utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira,
Changamoto na Mafanikio
Katibu Mkuu wa Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amezindua ripoti ya 15 ya utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini iliyoandaliwa na Mamlaka ya Uthibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Akizungumza jijini Dodoma, Mhandisi Mwajuma amesisitiza umuhimu wa kupunguza upotevu wa maji nchini, akieleza kuwa baadhi ya mamlaka zinapoteza asilimia 37.2 za maji yanayozalishwa, huku kiwango kinachokubalika kikiwa chini ya asilimia 20.
Aliongeza kuwa elimu ya kuvuna maji ya mvua ni muhimu kwa kukabiliana na uhaba wa maji, na kueleza umuhimu wa kufuata malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya mwaka 2030, hasa Lengo Namba 6 linalohusu Majisafi na Usafi wa Mazingira.
Mamlaka ya EWURA imepewa jukumu kubwa katika kufanikisha lengo hilo.
Ripoti hiyo inaonesha kuwa baadhi ya viashiria vya utendaji wa mamlaka za maji vimeimarika ikilinganishwa na miaka iliyopita, huku Mamlaka 78 kati ya 85 zikipata alama nzuri katika utendaji wao.
Hata hivyo, kuna changamoto za kuzorota kwa baadhi ya viashiria, kama upotevu wa maji ambao umeongezeka kutoka asilimia 35.5 hadi 37.2.
Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile, aliongeza kuwa mamlaka za maji zimeendelea kuimarika kwa kufikia malengo mbalimbali, kama kuongezeka kwa kiwango cha ubora wa maji na idadi ya wateja wa maji.
Uzinduzi huo pia ulikwenda sambamba na utoaji wa tuzo kwa mamlaka zilizofanya vizuri katika utoaji wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira.



0 Comments:
Post a Comment