TAWIRI YABAINISHA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA TAFITI ZA WANYAMAPORI NCHINI
Ikiwa Kauli mbiu ya siku ya wanyamapori duniani 3 Machi, 2024 ni "Unganisha Watu na Ulimwengu: Vumbua Matumizi ya teknolojia Katika Uhifadhi wa Wanyamapori " Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI ) imebainisha matumizi ya teknolojia yanavyorahisisha tafiti za wanyamapori nchini.
Akizungumza na Mwanahabari wetu, Mkurugenzi Mkuu TAWIRI, Dkt. Eblate Ernest Mjingo amesema teknolojia mbalimbali zimerahisisha tafiti za wanyamapori nchini kufanyika kwa wakati na kwa usahihi zaidi.
Dkt. Mjingo amebainisha miongoni mwa teknolojia zinazotumika katika tafiti za wanyamapori ni pamoja na matumizi ya tekinolojia ya akili mnemba (artificial intelligence) kuchakata takwimu na uchambuzi wa picha katika zoezi la kuidadi wanyama (sensa), teknolojia ya mikanda ya visukuma mawimbi( GPS satellite Collar) kufuatilia mienendo ya wanyamapori, matumizi ya ndege zisizo na Rubani rubani (Drone)kutatua changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu .
Pia, matumizi ya helikopta/ndege kuwafuatilia wanyamapori kwa matibabu au kuwarejesha wanyama maeneo ya hifadhi, kamera za kutega (camera trap) kubaini aina ya wanyamapori waliopo katika maeneo mbalimbali na changamoto za uhifadhi na tekinolojia ya vinasaba (DNA) kutambua afya ya uzazi wa wanyamapori kwenye mifumo ikolojia mbalimbali.
Dkt. Mjingo amesema awali kabla ya matumizi ya teknolojia kulikuwa na ugumu katika kufanya tafiti za wanyamapori baadhi ya maeneo kwani iliwalazimu watafiti kutumia muda mrefu kufanya tafiti, kutumia gharama kubwa, usalama mdogo .
" kwa kutumia teknolojia ya Akili mnemba (AI) kuchambua picha na kuchakata takwimu imesaidia kutumia nusu ya siku zilizokuwa zimatumika awali sambamba na kupunguza gharama " ameeleza Dkt. Mjingo
Vilevile Dkt.Mjingo amebainisha awali ilikuwa vigumu kuwafuatlia tabia za wanyamapori kwani wanyamapori wakiona gari au watu mara nyingi hubadili tabia sambamba na ugumu kufuatilia wanyamapori nyakati za usiku, msimu wa mvua na maeneo yasiyo fikika ambapo kwa sasa teknolojia ya kamera za kutega (camera trap) inatumika nyakati za mchana na usiku.
Aidha, Dkt.Mjingo ametoa wito kwa wadau wa uhifadhi na utalii ndani na nje ya nchi kushirikiana na TAWIRI kwa kuzingatia tafiti za wanyamapori ni muhimu katika sekta ya uhifadhi na utalii nchini ambapo pia ametoa wito kwa mamlaka za uhifadhi kutumia ushauri wa kisayansi unaotokana na matokeo ya tafiti mbalimbali.
0 Comments:
Post a Comment