NCHI NNE KUJA KUJIFUNZA TANZANIA MABORESHO HUDUMA ZA POSTA

 


BAADA ya Tanzania kupiga hatua katika kutumia teknolojia ya mawasiliano ikiwemo utumiaji wa simu ya kiganjani kuagiza mizigo mbalimbali ndani na nje ya nchi na kuagiza chochote kwa kutumia teknolojia hiyo, bila usumbufu wala kupoteza muda hali iliyozisukuma nchi nne za Umoja wa Posta Afrika (PAPU),kuomba kuja kujifunza.


Nchi hizo ni Kenya, Burundi, Zimbambwe na Jamuhuri ya Demokrasia ya Kongo zimeomba kuja nchini kujifunza uboreshaji wa huduma za sekta ya posta uliofanywa na serikali, ili nao wakapeleke utaalamu huo kwenye nchi zao na kuleta maendeleo kwa Bara lote la Afrika.


Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania , Macrice Mbodo ameyasema hayo leo Agosti 31,2023 jijini Arusha kwenye kikao cha wasimamizi na watoa huduma wa sekta ya posta barani Afrika na nje ya mipaka ya  bara hilo ikiwa ni mwendelezo wa mikutano kadhaa iliyofanyika mkoani hapa. 


Kikao hicho kimewaleta pamoja wakuu wa taasisi hizo barani Afrika kwa lengo la kujadili kuona jinsi ya uboreshaji wa huduma za posta na kutatua changamoto wanazokutana nazo.


“Nchi zilizoomba kuja kujifunza hapa kwetu ni majirani zetu Kenya, Burundi, Zimbambwe na Jamuhuri ya Demokrasia ya Kongo. Lengo letu wote tutoa huduma zinazofanana katika bara letu hili," amesema Mbodo na kuongeza.


...Ndio maana kila nchi inapata uzoefu wa nchi zingine, hata sisi yapo mambo hatuyafahamu wenzetu wametutangulia, lakini nasi tumepiga hatua kubwa kwenye uboreshaji wa miundombinu yetu,”.


Amesema moja ya hatua iliyopigwa Tanzania kwa sasa ni utumiaji wa simu ya kiganjani,  katika uagizaji wa mizigo mbalimbali ndani na nje ya nchi na kuagiza chochote kwa kutumia teknolojia hiyo, bila usumbufu wala kupoteza muda.


Mbodo amesema  Shirika la posta kama sekta  haitakufa, hata zaidi ya miaka mia moja, kwa sababu watoa huduma wake wanaendelea kujipanga na kufanya mageuzi  ya kutosha kwenye utoaji wa huduma za, ili kusaidia maendeleo katika Bara la afrika.



Awali akifungua mkutano huo Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye  amesema kuwa kumekuwa na mikutano mbalimbali kwa makundi tofauti mkoani Arusha  ya  watoa huduma wa sekta ya posta barani Afrika, ili kubadilishana uzoefu  kwa ajili ya kuboresha zaidi  utoaji huduma zao.


“Lakini leo tutamalizia na kikao cha Mawaziri wa sekta ya posta kwenye bara letu hili na kumalizia na uzinduzi wa jengo la makao makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU), utakaozinduliwa na Rais Samia Hassan Suluhu Septemba 2 mwaka huu,”amesema Nnauye


Amesema  jengo hilo ni bora zaidi mkoani Arusha na ni moja ya kivutio kikubwa kwa wageni mbalimbali, hali hiyo imekua furaha kwa Taifa, kuona ndoto ya muasisi wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere  ya kuomba kujenga makao makuu hayo nchini imetimia.


Nnauye aliomba wananchi kujitokeza kuungana na Rais Samia, kwenye uzinduzi huo na kuonyesha ukarimu kwa wageni mbalimbali watakaofika mkoani humo.


0 Comments:

Post a Comment