ALIYEMUUA KIGOGO TANAPA AHUKUMIWA KUNYONGWA

 

Emmily Kisamo (aliyesimama) enzi za uhai wake


 

MAHAKAMA  imemuhukumu kunyongwa hadi kufa , mfanyakazi wa ndani, Ismail Swalehe Sang’wa, (28) baada ya kumkuta na hatia ya kumuua kwa kukata shingo kwa panga mwajiri wake, Emily Kisamo (52) ambaye alikuwa Afisa wa Intelijensia wa Shirika la Hifadhi za Taifa nchini, (TANAPA).

 

Uamuzi huo umetolewa leo Machi 13,2023  na Jaji Mfawidhi, Joachim Tiganga wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha wakati akitoa uamuzi kwenye shauri hilo la mauaji  namba 70/2022.

 

Amesema kuwa baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mahakama hiyo imejiridhisha pasipo na shaka kuwa Sang’wa alitekeleza mauaji hayo kwa kuzingatia ushahidi wa mashihidi 10 na vielelezo 24 vilivyowasilishwa mahakamani hapo na upande wa jamhuri.

 

Jaji Tiganga amesema kuwa mahakama hiyo ilizingatia ungamo la mshitakiwa huyo mbele ya msimamizi wa amani ambapo alikiri kutenda kosa hilo la mauaji.

 

Hata hivyo Jaji huyo ameeleza kuwa  mahakama haikuutilia maanani tetezi wa mshitakiwa, Sang’wa kwani hakuwasilisha kielelezo wala shahidi wa kuithibitishia mahakama kuwa hakuwa eneo la tukio siku mauaji hayo yalipotokea.

 

Kwenye shauri upande wa Jamhuri ulikuwa unawakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Janet Sekule, Grace Madikenya, na Charles Kagirwa huku mshitakiwa huyo akitetewa na wakili, Victor Bernad.

 

Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Sang’wa ambaye ni mwenyeji wa kijiji cha Sepuka wilayani Ikungi katika Mkoa wa Singida alimuua mwajiri wake, KIsamo, Desemba 18, 2015 kati ya  saa 2:30 asubuhi hadi saa 4:00 asubuhi nyumbani kwake mtaa wa  Corridor Area Uzunguni jijini Arusha.



Sang’wa alitekeleza mauaji hayo wakati marehemu, Kisamo akiwa anakunywa uji sebuleni ambapo mfanyakazi wake wa ndani huyo  alimvizia na kumkata shingo kwa kutumia panga na kisha kuchukua mwili wake na kuuweka kwenye gari la marehemu aina ya Nissan Mazda lenye namba za usajili T. 435 CSY.




Baada ya kuuweka mwili wa marehemu kwenye buti alilisafisha gari hilo kwa nje na kisha kuliendesha mpaka eneo la kikwakwaru “B” kata ya Lemara jijini Arusha ambapo alilitelekeza hapo na kisha yeye kuondoka.



Mara baada ya gari hilo kukaa mpaka saa 2:00 usiku ndipo baadhi ya wananchi wa eneo hilo walitoa taarifa polisi  ambapo askari wa doria walikwenda na kulichukua gari hilo kwa kulivuta mpaka kituoni.

 

Gari hilo lilitambuliwa na  mke wa marehemu, Caroline Lukumay (38) ambaye  alikuwa anamtafuta mume wake kwa njia ya simu bila mafanikio na alikuwa ameshatoa taarifa polisi.

 

Polisi  walimuomba mke wa marehemu funguo za akiba za gari hilo ambapo baada ya kulifungua ndipo walipouona mwili wa marehemu kwenye buti.

 

 


Mara baada ya Sang’wa kukamatwa alikiri kuhusika na mauaji hayo na kusema siku hiyo walikuwa wawili tu yaani yeye na mrehemu, KIsamo na alifanya hivyo kwa kuwa alikuwa na tamaa za fedha alizokuwa nazo marehemu ndani ya nyumba.



 Polisi walipopekuwa nyumba hiyo walibaini kuwepo kwa fedha taslimu Tsh. 4,294,000, simu tatu aina ya Sumsang na vocha za mtandao wa vodacom za shilingi 5,000o zenye thamani ya shilingi 70,000 ambapo vyote vilifukiwa kwenye banda la kuku.



Sang’wa alionyesha panga lenye damu ambalo alilihifadhi stoo pamoja na taulo nne kubwa, kitambaa cha mezani na suruali yake ambazo zilikuwa na damu na alizitumia yeye mwenyewe kupigia deki sebuleni baada ya tukio na kisha kuzificha kwenye migomba karibu na mabanda ya kuku.



 

0 Comments:

Post a Comment