KERO YA BARABARA, MAJI, STAKABADHI GHALANI ZAICHEFUA ACT

 


ARODIA PETER, KILWA


CHAMA cha ACT Wazalendo kimekerwa na ubovu wa miundombinu ya barabara, maji na mfumo mbovu wa soko la mazao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani katika Jimbo la Kilwa Kusini Halmashauri ya Kilwa mkoani  Lindi.


Kutokana na hali hiyo chama hicho kimeitaka Serikali kuchukua hatua kukabiliana na changamoto hizo zinazoathiri maendeleo ya wananchi.



Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu Ado kwenye ziara yake ya kata kwa kata inayoendelea katika Jimbo la Kilwa Kusini mkoani Lindi.


Hadi sasa, Ado amekwishatembelea kata  za Masoko, Kikole, Likawage, Nanjilinji, Kiranjeranje na Lihimalyao.


Akiwa Kata ya Nanjilinji, Kayibu mkuu huyo aliitaka Serikali kuchukua hatua kuifanyia ukarabati barabara ya Ngea, Likawage hadi Nanjilinji kwa kiwango cha Changarawe na kujenga barabara ya Kiranjeranje, Nanjilinji hadi Ruangwa kwa kiwango cha lami.


"Nimesafiri usiku kutoka Likawage hadi Nanjilinji. Nimesikitika sana. sijawahi kuona njia mbovu kama hiyo. Hakuna atakayeamini kuwa hiyo ndiyo njia inayoelekea katika eneo linalozalisha ufuta bora zaidi nchini na kuingiza ushuru wa zaidi ya Sh milioni 600 kwa mwaka. Hili halikubaliki"alisema  Ado.



Aidha akiwa katika Kata ya Lihimalyao, Ado pia ameitaka Serikali kuchukua hatua za haraka kukabiliana na uhaba mkubwa wa maji.


"Serikali isikie, watu wa Lihimalyao wanaishi kwa shida kubwa kwa sababu ya maji, watu wanashindwa kuoga na maji ya kunywa ni machungu. Ndugu yangu Juma Aweso, (Waziri wa Maji), kama tuliweza kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria kwenda mikoa mbalimbali ya Kanda ya ziwa tunashindwa kuvuta maji kutoka Mikoma kwenda Lihimalyao?"alihoji  Ado. 


Aidha kiongozi huyi wa ACT Wazalendo mbali na hayo, kwenye  kata zote alizotembelea, alipokea changamoto za wakulima wa ufuta na korosho hasa kuhusu kushindwa  kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kuwapatia wakulima soko la uhakika la mazao.


"ACT Wazalendo imesikia kilio cha wakulima wa korosho na ufuta. Mmesema wazi kwamba hamuitaki stakabadhi ghalani kwa sababu hamlipwi vizuri na kwa wakati. Bila shaka Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe atazipata salamu zenu. Kama hawawezi kuzikabili changamoto za stakabadhi ghalani bora kurejesha soko la ushindani" alisisitiza Ado.


Leo Julai 12, 2022 Katibu mkuu huyo   atafanya ziara kwenye Kata za Pande na Mandawa na kuhitimisha ziara yake kesho kwa kufanya kikao na wanachama wa Kata ya Kivinje.

Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaib akisalimiana na mmoja wa wazee katika moja ya kata zilizopo Kilwa Kusini.


Kwenye ziara hiyo, Katibu Mkuu ameambatana na Katibu wa Sera na Utafiti, Idrisa Kweweta na viongozi wa Mkoa wa Lindi na Jimbo la Kilwa Kusini.


0 Comments:

Post a Comment