DPP AWACHOMOA WATATU KESI MAUAJI YA ASKARI LOLIONDO

MKURUGENZI wa Mashitaka Nchi, (DPP) amewaondoa washitakiwa watatu kwenye kesi ya kula njama na kumuua askari polisi mwenye namba G 4200 Koplo Garlus Mwita.

Kesi hiyo inayofuatiliwa wengi ndani na nje ya nchi na ilikuwa ikiwakabili washitakiwa 27 ambapo kwa sasa wamebaki washitakiaa 24.

Washitakiwa hao ambao DPP amesema hana nia ya kuendelea na mashitaka dhidi yao  ni pamoja na mzee, Lekeranga Koyee mwenye matatizo ya figo,  wanafunzi  wawili, Fred Victor anayefanya mafunzo ya uzamili, (PHD) nchini Marekani, na Simeli Parmwati anayetakiwa kujiunga na kidato cha sita.

Hati hiyo ya DPP imewasilishwa mahakamani leo na Wakili wa Serikali, Upendo Shemkole mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Fadhili Mbelwa, Daniel aliyeahirisha shauri hilo la mauaji namba 11/2022 baada ya Haki Mkazi, Herieth Mhengaambaye shauri hilo huwa mbele yake kuwa na udhuru.

Hata hivyo uamuzi huo wa DPP umekuja siku ambayo  hakimu Mhenga alitazamiwa kutoa uamuzi mdogo juu ya hoja za kisheria zilizowasilishwa mahakamani hapo na mawakili wa utetezi wakitaka upelelezi wa kesi hiyo ukamilike mara moja ili kuwezesha washitakiwa kupata haki ya kusilikizwa kwenye mahakama yenye mamlaka ya kusikiliza shauri hili.

Pia walitaka washitakiwa wawili waweze kupata haki yao ya kupata elimu na wengine wawili wapatiwe haki ya kupata huduma za afya ambapo watatu kati yao wamechiwa huru huku mshitakiwa namna 19, Kijooli Kakeya anayesumbuliwa na ugonjwa wa Kisukari akisalia kwenye shauri hilo
 

"Upande wa Jamhuri wanahoja ya kuieleza mahakama kuwa Mkurugenzi wa mashtaka, (DPP) hana nia ya kuendelea kuwashtaki washtakiwa watatu kwenye shauri hili mshtakiwa 3 Simeli   Parmwati, mshitakiwa wa  22 Lekeranga Koyee na mshitakuwa wa 23 Fred victor kwa sababu hiyo wanaomba kuwaondolea mashtaka," alieleza wakili wa Serikali  Shemkole.

Kwa upande wake, Wakili wa Wakili Myela, alipongeza uamuzi huo wa kuwaachia huru washitakiwa hao watatu lakini akahoji sababu za mshitakiwa namba 19, i Kakeya anayesumbuluwa na ugonjwa wa kisukari kuendelea kushitakiwa wakati wao waliwasilisha maombi ya wote kupatiwa matibabu.

 
Hata hivyo Hakimu  Mbelwa alihoji endapo kama kuna pingamizi lolote kwa upande wa utetezi juu ya washitakiwa   hao watatu kufutiwa mashtaka ambapo upande wa utetezi wakiongozwa na wakili Myela walisema hawana pingamizi lolote 

Hakimu huyo aliwaambia washtakiwa hao kuwa jamhuri haijaona kama  wanamashtaka na mahakama na kwa kuwa imeona  hakuna pingamizi kwa hivyo  inawaondolea mashtaka hayo na kuwaachia huru hivyo wanaobaki washtakiwa 24 katika Kesi hiyo .


Hata hivyo wakili wa utetezi, Myela aliendelea kusisitiza mahakamani hapo kuwa  wanaomba majibu thabiti kuhusu mshtakiwa namba 19 ambaye wakili wa jamhuri alisema atatoa majibu kuhusu mshtakiwa huyo na kwakuwa magereza hawana dawa anazotumia na anaendelea kuathirika hivyo wanaomba ifanyike utaratibu utakaomweka salama na mleta mashtaka alikubali 

Akijibu hoja hiyo, Wakili wa jamhuri, Shemkole ameeleza kuwa ni kweli jambo liliongelewa kwa washtakiwa ambapo aliahidi  kuyachukua na kuyafanyia kazi hivyo kwa huyo aliyebaki upelelezi bado unaendelea na endapo ukikamilika kwa wakati mwingine atakuja na majibu 



Kwa Upande wa utetezi, Jebra Kambole, ameiomba upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi kwa wakati kwa kuwa shitaka linalowakabili halina dhamana na kila mtu aliyepo ndani anachangamoto zake na kila mtu akisema changamoto zake hawawezi kumaliza shtaka hilo hivyo upelelezi ufanyike kwa haraka ili aliyetenda kosa hilo achukuliwe hatua na wengine waendele na majukumu yao.


Hakimu  Mkazi Mfawidhi,  Mbelwa amesema upande wa jamhuri umesikia hoja hizo hivyo akaahirisha shauri hilo mpaka Agosti 5, mwaka huu siku ambayo hakimu Mhenga anatarajiwa kutoa uamuzi mdogo endapo mahakama hiyo inaweza kuendelea kusikiliza shitaka la kula njama.

Washitakiwa wengine kwenye shauri hilo ni pamoja na Molongo Paschal, Albert Selembo,  Lekayoko Parmwati, (21) Sapati Parmwati, (30) Ingoi Olkedenyi Kanjwel, (20) Sangau Morongeti, (Morijoi Parmati, (20) Morongeti Meeki, (Kambatai Lulu,(40) na  Moloimet Yohana,(37)?

 

Wengine ni  Ndirango Senge Laizer, (52) Joel Clemes Lessonu, (54)  Simon Nairiam Orosikiria, (59)  Damian Rago Laiza, Mathew Eliakimu, (41) Luka Kursas, (49)  Taleng'o Twambei Leshoko, (37) Kijoolu Kakeya, (56)   Shengena Killel, (34) Kelvin Shaso Nairoti, (33) , Wilsom Tiuwa Kiling, (32), James Mumes Taki (28), Simon Saitoti, (41), na Joseph Lukumay



Awali Julai 14, mwaka huu Wakili wa Serikali Shemkole aliwasomea upya washitakiwa hao makosa yao ambapo alidai kuwa kuwa kosa la kwanza ni kula njama ya mauaji ambalo linawakabili  washitakiwa wote ambapo wanadaiwa katika tarehe na sehemu isiyofahamika walipanga njama ya kuua maafisa wa serikali na polisi  waliokuwa wakishiriki kuweka mipaka kwenye Pori Tengefu la Loliondo.


Katika shitaka la pili la mauaji wakili huyo wa serikali alidai  kuwa mnamo tarehe 10 Juni 2022 katika  eneo la Ololosokwan wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha kwa nia ovu washitakiwa hao walisababisha kifo cha askari polisi mwenye namba G 4200 Koplo Garnus Mwita.

HOJA ZINAZOSUBIRI UAMUZI MDOGO WA MAHAKAMA

Mawakili wa utetezi walidai kuwa kwa mujibu wa sheria  shitaka la kula njama halifunguliwi mahakamani mpaka ushahidi uwe umekamilika hivyo wakataka shtaka hilo lisikilizwe wakati upelelezi wa shitaka la mauaji likiendelea kuchunguzwa.

0 Comments:

Post a Comment