MAMLAKA ya manunuzi ya umma nchini,(PPRA)wametakiwa kuwa makini katika kusimamia na kufanya ukaguzi wa manunuzi na Ugavi wa bidhaa mbali mbali za miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini ili kutumia fedha za walipa kodi kikamilifu.
Hayo yamesemwa leo, Mei 7, 2022i na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, kwenye hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mstahiki meya wa jiji la Arusha, Maximilian Iranqhe akifunga kongamano la wiki ya ununuzi wa umma jijini hapa.
Amesema kuwa ni ununuzi wa umma ni muhimu uzingatie misingi na uadilifu wa fedha za umma na kusaidia kukuza uchumi wa nchi na kuepuka ujanjaujanja ambao ni kinyume na maadili ya utendaji wa umma.
"Tunaweza kuwa na sheria na mifumo mizuri ya TRHAMA lakini kama watendaji hawatakuwa waadilifu na wazalendo katika kutekeleza majukumu yake hatutaweza kukomesha vitendo vya ubadhirifu kwenye manunuzi," amesema Iranghe na kuongeza.
"Niwaombe muwe waadilifu katika kusimamia manunuzi ya umma kupitia miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini kwa lengo la kuokoa fedha za serikali za walipa kodi kwa ni kwa kufanya hivyo thamani ya fedha itaonekana kupitia bidhaa husika,".
Naye, Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya wiki ya ununuzi wa umma ambaye pia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Dkt Irene Isaack alisema katika kongamano hilo wameazimia maazimio 11 yaliyolenga kuongeza tija katika ununuzi ya serikali sambamba na kufanya tasmini kabla ya manunuzi
Dkt. Isaka alisema maazimio hayo yanalenga katika suala zima la uadilifu katika ununuzi wa umma ambao unaupunguzia gharama ya manunuzi katika serikali ikiwa lengo ni kuongeza tija pamoja na kuokoa fedha za walipa kodi za watanzania.
"Kwa hiyo kuna maazimio kwa upande wa mifumo ambayo inahitaji kufanya manunuzi kwa kutumia mifumo kuepuka matumizi ya kila taasisi kujiundia mifumo yao hivyo serikali mtandao imetakiwa kuhakikisha mifumo hiyo inazungumza,"akisema Mtendaji Mkuu.
Pia alisema maelekezo mengine ni pamoja ya kufanya tathmini ya kutosha kabla ya kufanya manunuzi ili kuepuka kununua bidhaa kwa gharama mara mbili ya ile ambayo iliyokusudiwa.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa chuo cha uhasibu Arusha,(IAA), Cairo Mwaitete alisema wao kama taasisi inayowaandaa wataalam wa manunuzi wanasisitiza katika kuangalia manunuzi ya umma yanaambatana na maadili hivyo ni wajibu wao kama chuo kuwaandaa vijana kuzingatia weledi na maadili ya manunuzi.
"Maadili ndio suala la msingi linaonyesha thamani ya fedha hivyo ni vyema tukajitahidi katika suala la manunuzi tuweze kuwaandaa vijana watakaokuwa na maadili ya manunuzi ikiwa sehemu kubwa ya bajeti ya Taifa kwa asilimia 80 ni manunuzi tu," alisema Mwaitete.
Kwa upande wake, Meya wa Jiji la Ilala, Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto alisema ni vema madiwani wakapatiwa mafunzo waweze kuelewa vema suala zima la manunuzi ya umma kwani wao ndiyo wanapitisha mipango ya halmashauri.
Naye, Mwenyekiti wa kamati ya tenda makao makuu ya Wakala wa Barabara nchini, (TANROADS), Hija Malamla amesema wanaelewa u uhimu wa kikao hicho ndiyo sababu wakaleta washiriki 67 ambao ni wengi ukilinganisha na taasisi nyingi
Aidha, Kamishna wa Idara ya Sera ya Ununuzi wa Umma Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Frederick Mwakibinga, amewataka wadau wa sekta ya ununuzi wa umma nchini kutoa mawazo kuwezesha maboresho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ili kuleta tija kwa Serikali.
‘’Tunaendelea kukusanya maoni kutoka makundi mbalimbali na watu wote ambao wanadhani nini kifanyike ili Sheria iweze kutekelezeka na iweze kunufaisha nchi, hili ni jukumu letu kuhakikisha kuwa eneo la ununuzi wa umma lina sera, Sheria, kanuni na miongozo inayokuwa na tija kwa Taifa’’ alisema Dkt. Mwakibinga.
Alisema Sheria ya ununuzi wa umma inalinda maslahi ya Taifa kwani inawapa wananchi pamoja na wafadhili imani na Serikali katika matumizi ya fedha hivyo matumizi ya sheria hayapaswi kuingiliwa na mashinikizo.
Dkt. Mwakibinga alisisitiza maafisa manunuzi nchini kusimama katika sheria, kufanya kazi kwa nidhamu, kuheshimu taratibu za ununuzi na kuepuka kukiuka matumizi ya sheria kutokana na shinikizo lolote na kuwasiliana na wizara endapo watakutana na changamoto ya shinikizo la aina yoyote.
Aidha, Dkt. Mwakibinga alisema kuwa Wizara imetoa kanuni za maadili kwa wote wanaoshiriki katika ununuzi wa umma ili kuweza kuwajumuisha wote wanaoshiriki katika ununuzi wa umma kwa kuwa maamuzi yao huathiri ununuzi wa umma.
Kongamano la Wiki ya Ununuzi wa Umma limeandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango na taasisi zinazosimamia ununuzi wa umma nchini ambazo ni Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini (GPSA), Mamlaka ya Rufaa za Zabuni za Umma (PPAA) na Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB).


0 Comments:
Post a Comment