Thursday, May 5, 2022

DALADALA ARUSHA ZAGOMA, WANANCHI WAPANDA GUTA

 

 


 

MGOMO wa magari ya abiria jijini kupinga ongezeko la bei ya mafuta huku kiwango cha nauli kinachotozwa kikiwa ni  kilekile umesababisha adha kubwa kwa watumiaji wa huduma hiyo ambao walilazimika kutembea umbali mrefu huku wakitumia usafiri wa pikipiki piki za wazi zinazotumia matairi matatu 'guta'.

 

 

Aidha, hali hiyo imemlazimu Mkuu wa wilaya ya Arusha, Said Mtanda kufika kwenye kituo cha magari ya abiria cha Kilombero kuzungumza na madereva hao na kuiagiza Mamlaka ya kudhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kujadili na madereva hao.

 



 

 

Tukio hilo limetokea leo  majira ya asubuhi ambapo madereva hao walisema kuwa wanahitaji bei za nauli ziongezwe walau zifike shilingi 600 au 700 tofauti na shilingi 400 inayotozwa sasa.

 

 

"Tumeanza kutoza nauli ya shilingi 400 tokea bei ya mafuta ikiwa shilingi 1,700 na bado tunaambiwa tuendelee na nauli hiyohiyo wakati tunanunua mafuta kwa bei ya zaidi ya shilingi 3,000 kwa lita," amesema mmoja wa madereva ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja.

 

 

Amesema kuwa wana wana familia zinazowategemea hivyo wanafanya kazi hiyo kwa malengo ikiwemo kufikia kiwango walichopewa na matajiri baada ya kutoa gharama za uendeshaji jambo alilodai kwa bei ya mafuta ilivyopanda ni ngumu kuweza kufikia kiwango hicho.

 

 

Kwa upande wao abiria wameelezea usumbufu mkubwa waliopata wa kusubiri usafiri muda mrefu bila mafanikio hivyo kulazimika kutembea na wengine kupanda bajaji, guta na magari mengine madogo ya mizigo.

 

 

Wamesema kuwa wanafunzi ndiyo wamepata shida zaidi kwani hata hayo magari ya mizigo yalikuwa hayakubali kuwapakia kutokana na nauli yao ya shilingi 200 kuonekana kuwa ndogo zaidi.

 

 

 

LATRA ilitangaza ongezeko la shilingi 100a kwenye nauli ya awali ifikapo siku 14, huku ongezeko la bei ya Mafuta ikiwa imefikia Tsh 3321 kwa lita moja ya Mafuta ya Diseli.

 

 

Kikao cha LATRA na madereva hao kilizaa matunda baada ya mamlaka hiyo kuruhusu bei mpya ya nauli yenye nyongeza ya shilingi 100 kuanza kutumika tofauti na awali ambapo ingeanza kutumika mei 15, mwaka huu.

 

 

Hivyo mabasi madogo ya abiria yalirejea barabarani kuanzia majira ya mchana yakitoza nauli ya shilingi 500 tofauti na ile ya awali ya shilingi 400.

 

No comments:

Post a Comment