MGOMO wa magari ya
abiria jijini kupinga ongezeko la bei ya mafuta huku kiwango cha nauli
kinachotozwa kikiwa ni kilekile umesababisha adha kubwa kwa watumiaji wa
huduma hiyo ambao walilazimika kutembea umbali mrefu huku wakitumia usafiri wa
pikipiki piki za wazi zinazotumia matairi matatu 'guta'.
Aidha, hali hiyo imemlazimu Mkuu wa wilaya ya Arusha, Said Mtanda kufika kwenye kituo cha magari ya abiria cha Kilombero kuzungumza na madereva hao na kuiagiza Mamlaka ya kudhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kujadili na madereva hao.
Tukio hilo limetokea leo
majira ya asubuhi ambapo madereva hao
walisema kuwa wanahitaji bei za nauli ziongezwe walau zifike shilingi 600 au
700 tofauti na shilingi 400 inayotozwa sasa.
"Tumeanza kutoza
nauli ya shilingi 400 tokea bei ya mafuta ikiwa shilingi 1,700 na bado
tunaambiwa tuendelee na nauli hiyohiyo wakati tunanunua mafuta kwa bei ya zaidi
ya shilingi 3,000 kwa lita," amesema mmoja wa madereva ambaye jina lake
halikuweza kupatikana mara moja.
Amesema kuwa wana wana
familia zinazowategemea hivyo wanafanya kazi hiyo kwa malengo ikiwemo kufikia
kiwango walichopewa na matajiri baada ya kutoa gharama za uendeshaji jambo
alilodai kwa bei ya mafuta ilivyopanda ni ngumu kuweza kufikia kiwango hicho.
Kwa upande wao abiria
wameelezea usumbufu mkubwa waliopata wa kusubiri usafiri muda mrefu bila
mafanikio hivyo kulazimika kutembea na wengine kupanda bajaji, guta na magari
mengine madogo ya mizigo.
Wamesema kuwa wanafunzi
ndiyo wamepata shida zaidi kwani hata hayo magari ya mizigo yalikuwa hayakubali
kuwapakia kutokana na nauli yao ya shilingi 200 kuonekana kuwa ndogo zaidi.
LATRA ilitangaza
ongezeko la shilingi 100a kwenye nauli ya awali ifikapo siku 14, huku ongezeko
la bei ya Mafuta ikiwa imefikia Tsh 3321 kwa lita moja ya Mafuta ya Diseli.
Kikao cha LATRA na
madereva hao kilizaa matunda baada ya mamlaka hiyo kuruhusu bei mpya ya nauli
yenye nyongeza ya shilingi 100 kuanza kutumika tofauti na awali ambapo ingeanza
kutumika mei 15, mwaka huu.
Hivyo mabasi madogo ya
abiria yalirejea barabarani kuanzia majira ya mchana yakitoza nauli ya shilingi
500 tofauti na ile ya awali ya shilingi 400.


0 Comments:
Post a Comment