HALMASHAURI ya Jiji la Arusha, imemsimamisha kazi dereva wake aitwae Athuman Mohamed Magio, kwa tuhuma za kutumia gari la halmashauri hiyo kusafirishia dawa za kulevya.
Katibu wa baraza la madiwani Daktari John Pima, juzi aliliambia baraza la madiwani lililojigeuza kuwa ni kamati maalumu ya kujadili nidhamu ya mtumishi huyo .
Alisema kuwa dereva huyo anayeshikiliwa na jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro, alikamatwa akisafirisha dawa hizo wilayani Rombo Mei 2, mwaka ambapo siku hiyo ilikuwa ni siku ya mapumziko ya sikukuu ya Eid el fitri.
Pima, ambae pia ni mkurugenzi wa halmashauri ya Jjiji hilo, alisema kuwa Magio alikamatwa akiendesha gari la halmashauri aina ya Toyota landcruiser lenye namba za usajili STJ 7333.
"Asubuhi alitumwa kwenda wilayani Karatu kuwachukua maafisa wa halmashauri hiyo waliokuwa wilayani Karatu kwa shughuli za kikazi na aliporudi Arusha, aliegesha gari hilo kwenye ofisi za Jiji na kulikabidhi kwa walinzi kwa kuliandikisha kwenye kitabu cha walinzi," alisema Dkt Pima.
Alisema ilipofika jioni alirudi kuchukua gari hilo na kuwadanganya walinzi kwamba alikuwa akiendelea na kazi hivyo walinzi walimruhusu na kuondoka na gari hilo hadi wilayani Rombo alikokamatiwa na polisi waliokuwa doria.
Dkt Pima alisema kuwa kitendo alichofanya dereva huo ni kinyume na kanuni za utumishi wa ummma.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, (RPC), Simon Maigwa hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo baada ya simu yake ya kiganjani kuwa inaita muda wote bila kupokelewa.

No comments:
Post a Comment