WAFANYABIASHARA wenye maduka jijini Arusha wameandamana kupinga hatua ya wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga kurejea kupanga bidhaa mbele ya maduka yao.
Aidha Mkuu wilaya ya Arusha, Said Mtanda ameagiza wamachinga hao ambao awali walishapangiwa maeneo ya kufanya biashara zao wakamatwe na kuchukuliwa hatua sheria pindi wakikutwa kwenye maeneo wasiyostahili kuwa.
Maandamano hayo yalifanyika leo May 13, 2022 jijini Arusha kuelekea kwa Mkuu wa wilaya ambaye aliwaeleza waandishi wa habari kuwa wamachinga watakaokutwa wamepanga bidhaa kandokando ya barabara wachuuliwe hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.
"Serikali haijabadili msimamo wake kuhusu wamachinga, baadhi yao wanaorejea barabarani ni ukaidi tu na sisi kama viongozi tutaendelea kusimamia sheria na wale wakaidi wachache nimeagiza wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria," amesema Mtanda.
Awali mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara wenye maduka,jijini Arusha, Loken Adolph alisema kurejea kwa wamachinga na kupanga bidhaa zao kando ya maduka ya wafanyabiashara linatokana na msukumo wa wanasiasa kinyume na maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Alisema kuwa tatizo hilo litaisha pale viongozi katika jiji la Arusha ambao (hakuwataja kwa majina) wakiacha siasa na badala yake wasimamie sheria katika kutekeleza majukumu yao.
Locken alisema kuwa serikali iliweka utaratibu mzuri kwa kutenga maeneo ya machinga na kuwahamishia huko ili kuondoa msongamano mjini na kuwapa nafasi wafanyabiashara wenye maduka wanaolipa kodi mbalimbali za serikali kuuza bidhaa zao kwa uhuru.
"Kwenye mambo ya msingi tuache siasa ,suala la wamachinga lilishamalizwa na Rais Samia kwa kuagiza wamachinga wapangiwe maeneo yao sasa inakuwaje wameanza kurejea na viongozi wapo kimya, tunatoa muda hili jambo likomeshwe na warudi kwenye maeneo yao,"alisema Locken.
Hata hivyo mwenyekiti wa Machinga jijini Arusha, Amina Njoka alisema suala la machinga linapaswa kutazamwa kwa mapana zaidi kwani baadhi ya wafanyabiashara wa maduka wamekuwa wakiwatumia a kuuza bidhaa zao kando ya maduka yao.
Alisema hakubailiani machinga kurejea barabarani ila anaamini kwamba kurejea kwa machinga barabarani kuna msukumo wa baadhi ya wafanyabiashara wanaowatuma kuwauzia bidhaa zao.
Kwa upande wao baadhi ya wamachinga hao walidai sababu ya kuamua kureja kando ya barabara zilizo katikati ya jiji ni kuwa maeneo waliyohamishiwa hayana wateja kwani hayafahamiki .
) ,Ridhiki Omari na Stella Francis walieleza kuwa maeneo ya soko waliohaishiwa kufanya biashara zao hayana wateja ndio maana wameamua kurejea barabarani.
"Maeneo ya masoko tuliotengewa liliwemo soko la Machame na Ulezi sio rafiki kwa biashara kwa kuwa hakuna mteja anayepita huko ndio maana tunakuja mtaani kuwafuata wateja "alisema Stella Fransis.
Mmachinga mwingine, Riziki Omary alisema kuwa kwenye maeneonwaliyohamishiwa biashara imekuwa ngumu kwani hakuna wateja wanaofika kwa ajili ya kununua bidhaa.
Maeneo yanayodaiwa kuvamiwa na machinga ni pamoja na soko la Kilombero, barabara ya Chini ya Mti, Soko na Kuu ambapo wamekuwa wakiweka bidhaa kanfo ya barabara hivyo kuziba maduka ya wafanyabiashara.
Wamachinga hao wamekuwa wakianza kurejea majira ya saa tisa alasiri ambapo kwenye mtaa wa kati wale wanaouza vyakula wamekuwa wakiweka majiko na kuendelea kupika vyakula mbalimbali wanavyouza.
No comments:
Post a Comment