Thursday, May 12, 2022

ALIYEACHIWA PAMOJA NA SABAYA ATOKA GEREZANI

 



HATIMAYE, Daniel Mbura aliyekuwa amefungwa pamoja na Lengai Ole Sabaya amechiwa huru kutoka gerezani baada ya Mahakama Kuu kanda ya Arusha kubatilisha na kufuta kifungo cha miaka 30 walichokuwa wakitumikia.

Wakili wa Mbura, Moses Mahuna ameieleza Tanzania Daima kwa njia ya simu kuwa mteja wake huyo aliachiwa huru juzi, kutoka kwenye gereza la Kisongo  alipokuwa akitumikia kifungo hicho.

Mbura ametoka gerezani baada ya taratibu za kimahakama kupeleka hati ya kuachiliwa kukamilika siku nne baada ya mahakama kuu kanda ya Arusha kumuachia huru Mei 6, mwaka huu pamoja wenzake, Sabaya na Silvester Ngegu ambao wameendelea kubaki mahabusu kwenye gereza hilo kutokana na kujabiliwa na kesi nyingine ya uhujumu uchumi ambayo haina dhamana.

"Magereza walikuwa wanasubiri mahakama imalizie taratibu za kuandika hati ya kutolewa magereza (remove order)  kwa Daniel. imendikwa na msajili wa mahakama kuu jumatatu ( 9 Mei, 2022) ikafika kwa mkuu wa magereza jana ( mei10, 2022)  akaachiwa," alieleza wakili Mahuna kwa njia ya simu.

Hata hivyo Mkuu wa gereza la Kisongo, Felix alipoongea na Tanzania Daima kwa njia ya simu alisema kuwa yeye si msemaji atafutwe Kamanda wa magereza mkoani Arusha.

Awali mei 6, mwaka huu,Jaji, Sedekia Kisanya wa mahakama Kuu Kanda ya Musoma aliyesikiliza shauri hilo la rufaa namba 129/2021 kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Arusha aliwaachia huru waleta rufaa wote watatu .

 

“Kwa upande wangu naona haya mapungufu ya mkanganyiko kwenye ushahidi zile ground nyingine nakubaliana na maombi ya waleta  rufaa, nabatilisha mwenendo na hukumu zilizotolewa dhidi ya waleta rufaa,” alisema Jaji huyo akitoa amri na kuongeza.

 

“ Naamuru waleta rufani waachiliwe huru,  waachiliwe huru isipokuwa kama wana mashauri mengine yasiyo na dhamana waendelee nayo,” .

 

Jaji Kisanya alitoa uamuzi huo kunzia majira ya saa 6 mchana ambapo upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili wa serikali mwandamizi, Felix Kwetukia huku upande wa waleta rufaa ukiwakilishwa na mawakili Moses Mahuna, Faudhia Mustafa, Sylvester Kahunduka, Gabriel Rwahira, Edmund Ngemela na Fridolin Gwemelo.




No comments:

Post a Comment