SERIKALI yaridhishwa na uhifadhi
na hatua zilizochukuliwa na kampuni
ya Raha beverages limited inayozalisha mvinyo na Kampuni ya Bia nchini,(TBL)
jijini Arusha, walivyoboresha mifumo yao ya maji taka hivyo kuwa salama kwa
mazingira na afya za watu wanaozunguka viwanda hivyo.
Aidha wenye viwanda
nchini wametakiwa kuhakikisha wanaweka mifumo sahihi ya kisasa kudhibiti
maji taka yanayotoka kiwandani na kuacha kuyaelekeza kwenye makazi ya watu
hatua inayosaidia kuondoa uharibifu wa mazingira na kuleta madhara ya kiafya
Kwa binadamu.
Naibu waziri, ofisi ya
Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Hamad Hassan Chande ameyasema hayo leo alipotembelea
kampuni ya Bia nchini, (TBL) na Kampuni ya Raha Beverages .
Naibu waziri akiwa
ameambatana na viongozi wa NEMC Mkoani hapa,aliridhishwa na mfumo wa kudhibiti
Maji taka unaotumiwa na viwanda hivyo ambapo huchakata maji taka na kuyarejesha
upya kiwandani kwa ajili ya matumizi mengine ikiwemo umwagiliaji wa mimea jambo
ambalo amevitaka viwanda vingine kuiga mfumo huo.
Akiongea wakati akikagua
mtambo wa kuchakata Maji taka kiwanda cha Raha beverage, Naibu waziri, Chande
aliridhishwa na na hatua ya kiwanda hicho kwa kuweza kudhibiti Maji taka yasitiririke kuelekea
kwenye makazi ya watu hivyo akavitaka viwanda vingine kujifunza kutoka kampuni
hiyo.
Hata hivyo alisema ipo
dhana kwa baadhi ya viwanda kuwa kutiririsha Maji taka ya viwandani kwenye
makazi ya watu kwa madai maji hayo yamechakatwa na hayana madhara kwa binadamu
na mimea jambo alilosema kuwa watatuma wataalam wao kwenye maeneo hayo
wakafanyie utafiti ili kujiridhisha .
"Tutatuma wataalamu
wetu kwenye viwanda vinavyotiririsha Maji kwenye makazi ya watu wakidai maji
hayo hayana madhara ili wafanye uchunguzi na Serikali itatoa tamko, yapo
malalamiko mengi ya wananchi yanayohitaji majibu ya wataalamu,"amesema
Naibu Waziri Chande.
Kwa upande wake meneja
wa mauzo na masoko katika kiwanda cha Raha Bereveges , Daniel Olomi amemweleza
Naibu Waziri, Chande kuwa kiwanda hicho kinachotengeneza mvinyo aina ya
Raha ,kinatumia mfumo wa kisasa wa kudhibiti Maji taka yanayotoka
kiwandani ili kuweza kutumika Kwa matumizi mengine bila kuleta madhara.
Alisema Kampuni ya Raha
Bereveges wa muda mrefu imekuwa ikitumia mfumo huo wa kisasa wa kusafisha Maji
taka ya kiwandani ili kuweza kutumika Kwa ajili ya umwagiliaji wa mimea bila
kuwa na madhara .
“Maji yetu yanapimwa na
watu wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Arusha,(AUWSA) na Baraza la Taifa la
Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira, (NEMC) na wamethibitisha maji yetu ni salama
hayana madhara kwa mwanadamu na yanaweza kutumika kwenye umwagiliaji wa mime,”
amesisitiza Olomi na kuongeza.
“Sisi tunazalisha mvinyo , raha poa na raha gold utokanao na ndizi na malighafi tunanunua
hapahapa nchini ikiwemo ndizi, sukari, hamira na tunaajiri wananchi hivyo mbali
ya kulipa kodi lakini tunachangia kutoa ajira zaidi,”.
Meneja rasilimali watu wa kampuni ya Raha Beverages limited, Beatha Antony.
“ Tunawaomba Watanzania nao watusapoti kwa kutumia vinywaji vyetu vyenye ubora wa hali ya juu uliothibitishwa na Shirika la viwango nchini, (TBS)na vina stamp ya kodi hivyo wanywaji wetu waangalie kwenye kizibo kuona kama zina stika hizo,” amesema Meneja rasilimali watu wa kampuni hiyo, (human resource) Beatha Antony.




0 Comments:
Post a Comment