MAHAKAMA YAELEZWA NAMNA SABAYA NA WENZAKE WALIVYOIBA KWA BUNDUKI



MAHAKAMA yaelezwa namna aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili walivyotumia bunduki kuwatisha watu waliokuwa kwenye duka la Shaad  kisha wakamfunga pingu Diwani wa Sombetini, Bakari Msangi, (CCM) na kumuibia shilingi 390,000.

Aidha inadaiwa kuwa waliwatisha watu hao kuwa watawavyatulia  risasi endapo wangeshindwa kueleza alipo mmiliki wa duka hilo, Mohamed Saad.

Wakili wa Serikali,  Tarsila Gervas aliieleza mahakama ya hakimu mkazi Arusha mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Salome Mshasha anayesikiliza shauri hilo la jinai shauri la jinai namba 66 la unyang'anyi wa kutumia silaha.

Kwenye shauri hilo linalovuta hisia za wengi upande wa Jamhuri unaongozwa na  Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Taifa ya Mashitaka ambaye ni Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka, wakili wa serikali mwandamizi, Abdallah Chavula na Wakili wa Serikali,  Gervas huku Sabaya na washitakiwa wengine watano wakitetewa na wakili maarufu jijini hapa, Moses Mahuna.

Wakili wa Serikali, Tarsila aliieleza mahakama hiyo kuwa Februari 9, mwaka huu washitakiwa hao Sabaya, Sylvester Nyengu na Daniel Mbura walivamia duka la Shaad lililopo mtaa wa biashara jijini Arusha.

"Walipofika waliwalazimisha watu wote kulala chini kwenye sakafu huku wakiwapiga kwa kutumia mateke, ngumi pamoja na makofi," Wakili wa Serikali Tarsila aliieleza mahakama nankuongeza. 

...Mshitakiwa wa kwanza, (Sabaya) aliwanyooshea bunduki wote huku akiwatisha kwamba atawafyatulia risasi kama wakishindwa kumweleza anayemiliki duka hilo yuko wapi...

..Lakini hawakumpatia jibu na badala yake mshitakiwa namba moja alimfunga kwa pingu mmoja wa watu waliokuwa katika duka hilo ambaye anaitwa Bakari Rahibu Msangi ambaye ni diwani wa kata ya Sombetini...

....Na akiwa ameshika silaha, bunduki ameshika mkononi alimtesa na kumtisha kumuua (Msangi) kwa kuwa alikuwa akitishia kuingilia biashara zake alizokuwa akifanya mahali hapo,". 

Wakili Tarsila aliendelea kuieleza mahakama hiyo kuwa washitakiwa wote kwa pamoja waliwapekua watu waliokuwa kwenye duka hilo huku wakiwa wamewashikia silaha ambayo ilikuwa ni bunduki na waliweza kuchukua fedha taslimu kutoka kwa Bakari Rahibu Msangi kiasi cha shilingi 390,000.

Pia walichukua simu aina ya tecno moja  na fedha taslimu shilingi 35,000 kutoka kwa Ramadhani Ayoub Rashid ambaye pia alikuwa ni mhanga aliyekuwa katika duka hilo.


"Baada ya kufanya unyang'nyi wa kutumia silaha waliondoka tukio hilo lilitolewa taarifa kwenye kituo cha polisi upelelezi ulifanyika kutokana na vitendo hivyo vya kifedhuli walivyofanya dhidi ya wahanga na watuhumiwa hawa waliweza kukamatwa maeneo tofauti ndani mkoa wq Arusha, Kilimanjaro na Dar es Salaam," wakili huyo wa serikali aliieleza mahakama.



Alidai kuwa  wakati washitakiwa hao wanafanyiwa mahojiano na polisi walikubali siku hiyo ya tarehe 9, februari, 2021 walikuwa kwenye duka hilo la Mohamed Saad ambapo baadaye waliletwa mbele ya  mahakama hiyo kwa makosa yanayowakabili.



Washitakiwa wote walikana maelezo hayo isipokuwa walikubali kuwa waliletwa mbele ya mahakama shauri hilo limeahirishwa mpaka Julai 2, mwaka huu litakaporudi kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa.

KESI YA UHUJUMU UCHUMI

Kesi ya  inayomkabili  Ole Sabaya wenzake wanne ilishindwa kuendelea mahakamani hapo baada ya upande wa jamhuri kuieleza mahakama kuwa upelelezi wa shauro hilo haujakamilika.


Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abdalah Chavula aliieleza mahakama hiyo jana mbele ya hakimu Mkazi Mfawidhi, Martha Mahumbuga anayesikiliza shauri hilo la uhujumu uchumi namba 27/2021.

Chavula aliiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa kwa shauri hilo kwani upelelezi bado haujakamilika.

Washitakiwa wengine ni msaidizi binafsi wa DC Sabaya, Sylivester Nyengu, (26) maarufu kama Kicheche, Enock Mnekeni, (41), Watson Mwahomange, (27) maarufu kama Maliamungu, John Aweyo maarufu kama Mike one na Daniel Mbura, (38).

Wakili wa Utetezi, Mahuna alieleza mahakama hiyo kuwa hana pingamizi na ombi hila isipokuwa anaomba apatiwe nakala ya hati ya mashitaka kwani hiyo ni mara yake ya kwanza amefika mahakamani kwa ajili ya kuwawasikilisha wateja wake.

Wakili Mwandamizi wa Serikali, Chavula alisema watampatia ila akaiomba mahakama kama inayo nakala wampatie jambo ambalo hakimu aliridhia hivyo akampatia nakala hiyo.

Shauri hilo liliahirishwa mpaka Julai 2, litakapokuja kwa ajili ya kutajwa.


Awali Juni 4,mwaka huu Sabaya na wenzake watano walifikishwa mahakamani hapo majira ya saa saba mchana chini ya ulinzi mkali kisha wakasomewa mashitaka yao mbele ya mahakaimu wawili tofauti kisha wakarudishwa mahabusu kwenye gereza la Kisongo kutokana na kesi zinazowakabili kutokuwa na dhamana.


Mkurugenzi Msaidizi wa Mashitaka, Kweka aliieleza mahakama hiyo mbele ya hakimu Mkazi Mfawidhi, Martha Mahumbuga kuwa shitaka la kwanza ilidaiwa Ole Sabaya kuongoza genge la uhalifu kinyume cha sheria akishirikiana na washitakiwa wengine ambao si mtumishi wa umma 

ilidaiwa kuwa  mnamo Januari 20, mwaka huu katika maeneo mbalimbali ya jiji la Arusha Sabaya akiwa ni ofisa wa umma, mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro alikiuka majukumu yake ya kiofisi kwa pamoja akishirikiana na Mnikeni, Mwahomange, Aweyo na Nyengu.
 
"Kwa kujua na kwa malengo ambayo si halali kwa kutumia mamlaka yake kama afisa wa umma huyu mshitakiwa wa kwanza walijipatia manufaa ambayo ni kinyume cha sheria," Kweka aliieleza mahakama.

Katika shitaka la pili na tatu yanamkabili Sabaya peke yake ambapo anadaiwa kushiriki matukio ya rushwa ambapo mnamo Januari 20, mwaka huu katika maeneo ya jiji la  Arusha alishiriki vitendo vya rushwa kwa kumshawishi Francis Mrosso ampatie fedha kiasi cha shilingi milioni 90 kwa kumahidi kwamba atamsaidia kuweza kuepuka vitendo vya jinai vilivyokuwa vinamkabili ambavyo vilikuwa ni vya ukwepaji wa kodi.

Kweka aliendelea kuieleza mahakama hiyo kuwa katika shitaka la tatu Sabaya anadaiwa kuwa mnamo Januari 20, mwaka juu kwenye maeneo ya Mrombo jijini Arusha alipokea rushwa ya kiasi cha shilingi milioni 90 kutoka kwa Mrosso kwa maelezo kuwa angemsaidia kukwepa vitendo vya kijinai alivyodaiwa kukabiliwa navyo vya ukwepaji kodi .

 Katika shitaka la nne  linalowalabili washitakiwa wote watano ni la utakatishaji wa fedha haramu ambapo Ole Sabaya akishirikiana na Mnikeni, Mwahomange, Aweyo na Nyengu ambapo wanadaiwa januari 20, mwaka huu huko maeneo ya Kwamorombo, Jijini Arusha walijipatia kiasi cha shilingi milioni 90 wakati wakijua kuwa kujipatia fedha hizo ambazo ni mazalia ya uhalifu ilikuwa ni mwendelezo wa kosa la vitendo vya rushwa.

Washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwani mahakama hiyo haina nguvu kisheria kusikiliza shauri hilo ambapo upande wa jamhuri uliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa kwa shauri hilo kwani upalelezi bado haujakamilika.


UMATI WA WATU WAFURIKA NJE YA MAHAKAMA

Umati mkubwa watu ulikuwa nje ya mahakama hiyo kuanzia majira ya asubuhi wakisubiri basi la magereza liwalete Sabaya na washitakiwa wenzake.

Sabaya alifika mahakamani hapo majira ya saa tatu asubuhi ambapo mara baada ya kushuka kwenye basi mwananchi mmoja alimuita kwa sauti Sabaya ambapo naye alipunga mkono hewa.

Hali hiyo iliwafanya wananchi wachache kumshangilia huku idadi kubwa ya wananchi wakionekana na kusikika wakipaza sauti na kumuita 'Sabaya mwizi, jambazi muuaji' ambapo kelele hizo zilidumu mpaka alipoinhizwa kwenye mahabusu ya mahakama.

Aidha wakati Sabaya ma wenzake wakitolewa mahabusu wananchi hao walikuwa wakipaza sauti wakitaka Sabaya achuchumae kama washitakiwa wenzake jambo ambalo halikufanyika kwani askari magereza waliwapeleka kwenye chumba cha mahakama.

Hata wakati kesi hiyo ikiendelea wananchi hao walisikika wakipiga kelele akiwemo mama mmoja aliyesikika akisema kwa sauti ya kilio kuwa 'Sabaya Mungu yupo'.


MWISHO.




0 Comments:

Post a Comment