Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi (katikati), akiteketeza nyavu zenye matundu madogo kuashiria uzinduzi rasmi wa vita dhidi ya uvuvi haramu katika wilaya yake. |
TIMEANDIKWA NA KATUMA MASAMBA, habari leo
ANZANIA ni miongoni mwa nchi zinazofaidika na biashara ya uvuvi.
Mbali na uvuvi, pia inafaidika na utalii wa chini ya bahari unaofanywa na watu mbalimbali hasa wageni. Hata hivyo, biashara hiyo imeendelea kuingia dosari mbalimbali kutokana na uvuvi haramu unaosababisha kuadimika kwa samaki na hivyo, kuathiri uchumi na urithi wa nchi.
Licha ya juhudi za Serikali kutokomeza uvuvi huo haramu, bado wapo baadhi ya watu wanaoendelea kufanya uhalifu huo kwa kificho zaidi. Uvuvi haramu hutekelezwa kwa kutumia nyavu ndogo zilizopigwa marufuku, baruti na milipuko mingine.
Uhalifu huu unatajwa kuwa miongoni mwa mambo yanayosababisha kwa asilimia kubwa, kuharibu mazalia ya samaki na kusababisha samaki kukimbilia ukanda mwingine wa bahari. Manispaa ya Kinondoni ni miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na changamoto ya uvuvi haramu.
Inaelezwa kuwa, takribani milipuko 50 husikika kila siku katika ukanda wa fukwe za manispaa hiyo, hali inayotajwa kusababisha kukosekana kwa samaki na mazalia yake. Katika kukomesha uvuvi haramu katika fukwe za Manispaa hiyo, Serikali imeanza kupanga mikakati mbalimbali ya kuhakikisha inaukomesha.
Kadhalika, imekusudia kuweka nguvu kubwa kulinda fukwe zake kwa kuhakikisha Jeshi la Polisi linafanya doria katika maeneo mbalimbali na kuwakamata watu wanaojihusisha na uvuvi huo ili wafikishwe katika vyombo vya sheria.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi, anaeleza namna walivyopanga kuwadhibiti na kuwachukulia hatua wavuvi wanaojihusisha na uvuvi haramu katika fukwe za wilaya hizo ambazo ni Kunduchi, Mbezi Beach, Ununio, Msasani, Kawe na Mbweni.
Anasema uvuvi huo sio tishio kwa samaki peke, bali hata utalii wa chini ya bahari ambao umekuwa ukifanywa na baadhi ya watu hasa wageni wanaokuja nchini kufanya utalii wa mandhari ya chini ya maji. Kutokana na hilo, Hapi anaeleza azima ya Serikali katika kutokomeza zana haramu ambazo zimekuwa zikitumika katika uvuvi huo licha ya kupigwa marufuku na Serikali.
Anasema uvuvi huo ni hatari kwa kizazi cha sasa na baadaye. Anasema wavuvi hao haramu wamekuwa wakitumia nyavu zenye matundu madogo, mabomu, milipuko na kulipua matumbawe baharini ili kupata samaki.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, uvuvi huo umekithiri katika fukwe za manispaa hiyo na kuwa tishio na kwamba si tu uvuvi huo unaharibu mazingira, bali pia unaua samaki hasa wadogo na kusababisha mazalia yao kuharibika na hivyo, kutozaliwa tena.
Nyavu zenye matundu madogo huvua samaki wakubwa na wadogo wasiopaswa kuvuliwa hivyo kupunguza uzalishaji wa samaki katika sekta ya uvuvi. Mkuu huyo wa wilaya anasema, wameanza kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na uvuvi haramu, ili kuufanya ukanda wa bahari uliopo katika wilaya hiyo kuwa ni mahali salama.
“Uvuvi haramu ni jambo lisilokubalika duniani kote, tusipochukua hatua mapema litakuwa tatizo kubwa kwelikweli, tusimamie sheria na kuhakikisha hili suala la uvuvi haramu linabaki kuwa historia katika wilaya ya Kinondoni,” anasema Mkuu wa Wilaya.
Hapi ambaye pia alizindua rasmi kampeni ya kupambana na uvuvi haramu katika wilaya hiyo, amekabidhi majina 21 ya wavuvi haramu wakiwemo viongozi wanaojihusisha na uvuvi huo kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Suzan Kaganda.
Katika uzinduzi rasmi wa vita dhidi ya uvuvi haramu katika wilaya hiyo, Hapi aliteketeza zana za uvuvi haramu zenye thamani ya shilingi milioni 60, huku akitoa maagizo kwa vyombo vya usalama na watendaji wa serikali za mitaa kuhakikisha wanachukua hatua kali dhidi ya watakaobainika kujihusisha na uvuvi huo.
Anasema sheria ya uvuvi inaeleza wazi aina na vipimo vya nyavu za uvuvi zilizoruhusiwa katika kuvua samaki, hivyo kila mmoja anapaswa kuzingatia sheria hizo badala ya kuhatarisha mazalia ya samaki.
Anaongeza kuwa utumiaji wa zana haramu katika uvuvi una madhara mengi kwa watumiaji wenyewe ikiwemo wavuvi kupata ulemavu wa viungo vya mwili na wakati mwingine kupoteza maisha kutokana na milipuko ya mabomu wanayotumia.
“Wavuvi haramu wanatumia mabomu na milipuko, wanaua mazalia ya samaki, kama tusipochukua hatua mapema, watoto na vizazi vyetu hawatakula samaki. Hatuwezi kuvumilia hali hii iendelee, ukiacha tu hili la kumaliza mazalia ya samaki, lakini hata wale watalii wanaozamia chini ya bahari kuangalia mandhari hawatakuja,” anasema.
Anasema mbali na milipuko hiyo kumaliza mazalia ya samaki na kusababisha samaki kukimbilia ukanda wa mbali, lakini pia ni hatari kwa kuwa inaweza ikachangia kujitokeza kwa matukio ya uhalifu.
Ofisa Uvuvi wa Wilaya ya Kinondoni, Grace Katama alitoa ripoti juu ya uvuvi haramu katika Pwani za Manispaa hiyo akisema kuwa, katika kupambana na vitendo vya uvuvi haramu wamekuwa wakifanya doria za mara kwa mara katika nchi kavu, mialo ya samaki na baharini.
Anasema kupitia doria hizo wamefanikiwa kukamata zana mbalimbali haramu ambazo zimekuwa zikitumika katika uvuvi huo, ikiwemo nyavu zenye matundu madogo aina ya kokoro zipatazo 57 zenye urefu wa mita 10 kwa kila nyavu.
Anasema zana nyingine zilizokamatwa ni pamoja na mikuki 30 yenye thamani ya Sh 250,000, nyavu aina ya monofilament (ghost fishing gear) 20, pamoja na zana nyingine mbalimbali ambazo zote zilikamatwa katika kipindi cha kuanzia Septemba mwaka jana.
“Tumekuwa tukiendesha doria mbalimbali katika Ukanda wa Pwani ya Manispaa ya Kinondoni, ambayo ni Kunduchi, Msasani, Ununio, Mbweni na maeneo mengine ya manispaa yetu.” Anasema wameshakamata wavuvi mbalimbali wakiwemo wawili wanaotumia baruti waliofikishwa katika Kituo cha Polisi cha Kawe kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
Grace anafafanua kuwa pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanyika kudhibiti uvuvi haramu, wapo wavuvi wenye nia mbaya ambao wamekuwa wakifanya vitendo hivyo vinavyoathiri mazalia, makuzi na malisho ya samaki na viumbe wengine walioko baharini.
“Upungufu wa chakula hutokea kwa sababu samaki ni kitoweo kizuri na hivyo mazingira yakiharibiwa, samaki hawatapatikana kwa urahisi,” anasema Grace. Grace anashauri vita dhidi ya uvuvi haramu ipewe kipaumbele, huku akiwaasa viongozi kuwa mstari wa mbele katika kupambana na uhalifu huu.
Anasema, kwa kuwa uvuvi haramu ni aina ya uharamia wenye nguvu, juhudi na ushirikiano wa wananchi na vyombo vya dola zinahitajika ili kuwabaini wavuvi haramu na watu wanaojihusisha na biashara hiyo.
Anaongeza kuwa, ulipuaji wa baruti katika uvuvi ni tishio kubwa kwa Ukanda wa Pwani kwani miamba au matumbawe yanayolipuliwa ni kinga dhidi ya kasi kubwa ya mawimbi ya bahari yanayoiathiri vibaya pwani, hivyo jitihada zaidi zinahita- jika kudhibiti ulipuaji huo wa mabomu.
0 Comments:
Post a Comment