WABUNGE WANAWAKE WA JUMUIYA YA MADOLA (CWP) WATAKA JUMUIYA YA KIMATAIFA KUINGILIA UTEKWAJI WA WASICHANA NCHINI NIGERIA

WABUNGE wanawake wa Mabunge ya jumuiya ya Madola, (CWP), wameitaka jumuiya ya kimataifa kuingilia kati na kushirikiana na Serikali ya Nigeria kuhakikisha watoto wa kike zaidi ya 200 wanaoishikiliwa na kundi la kigaidi la Boko Haram wanaachiwa na kurudi kuungana na familia zao.

Aidha, CWP ukanda wa Afrika umepanga kwenda nchini humo kwa ajili ya kuongea na wanawake na Rais wa nchi hiyo, Goodluck Jonathan kujua ni jambo gani hasa limepelekea kutokea kwa hali hiyo iliyopelekea watoto kushikiliwa kusikojulikana kwa zaidi ya siku 200 sasa.

Hayo yalisemwa kwa nyakati tofauti jana jijini hapa na Mwenyekiti wa CWP, Rebeca Kidaga na Makamu Mwenyekiti wa CWP, Ukanda wa Afrika, Beatrice Shelukindo  wakati alipokuwa wakitoa misimamo wa vyombo hivyo katika mkutano mkuu wa Umoja wa Mabunge ya jumuiya ya Madola, (CPA), Kanda ya Afrika.

 

Kidaga ambaye pia ni spika wa bunge la Uganda alisema kuwa kama wabunge wanawake wameumizwa na tukio hilo hivyo wanawapa pole wazazi na familia za watoto hao huku wakitaka Serikali ya Nigeria na jumuiya za kimataifa kuhakikisha matukio  kigaidi ya Boko Haram yanakomeshwa .

Kwa Upande wake, Shelukindo ambaye pia ni mbunge wa Kilindi, (CCM), alisema kuwa wabunge wanawake ukanda wa Afrika watakwenda Nchini Nigeria kabla ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo unaotarajiwa kufanyika mwezi Aprili mwakani.

Awali akiwasilisha mada kwenye mkutano huo juu ya changamoto na mafanikio ya utekelezaji wa malengo ya milenia, kwenye elimu ya msingi kwa watoto wa kike, Shelukindo alisema kuwa hapa nchini imefanikiwa kwani kwenye baadhi ya maeneo idadi  wa watoto wa kike wanaojiunga na shule imekuwa sawa huku baadhi ya maeneo idadi ya watoto wa kike ikiwa kubwa zaidi.

 

Hata hivyo alisema kuwa suala la uhamasishaji wanawake kujiunga na masomo ya sayansi bado linakabiliwa na changamoto nyingi kutokokana na hulka na mazoea mabaya yaliyojengeka kwenye jamii kuwa wanawake hawawezi uhandisi sanjari na kutojiamini kwa wanawake.

 

"Kwa mfano ni vigumu kwa mwanamke aliyeolewa na  aliyeajiriwa na kampuni ya simu kutoka nyumbani kwake usiku kwenda kushughulikia tatizo lililojitokeza kwenye mitambo, mwaka 2009 kuna utafiti ulionyesha kwamba wanawake wanasayansi wanakwazwa na waume zao kutokana na utaratibu uliopo kuwa mwanamke husikiliza uamuzi wa waume zao na kuwaheshimu  hivyo  wamekuwa kikwazo," alisema Shelukindo.

 

Mkutano huu wa 45 wa CPA, Kanda ya Afrika unajuisha wajumbe 500 kutoka nchi 17 wanachama ambapo Spika wa bunge la Tanzania, Anne Makinda ni Rais wa taasisi hiyo.

 

 

 

 

 

Chombo hicho hufanya mkutano wake mara moja kwa mwaka ambapo nchi inayojitolea kuandaa mkutano wa mwaka unaofuata hupewa fursa ya kukiongoza kwa mwaka mmoja ambapo baada ya Tanzania, spika wa bunge la Lesotho, Sephiro Motanyane ambaye kwa sasa ni makamu wa Rai atakabidhiwa rasmi uongozi wa chombo hicho.

0 Comments:

Post a Comment