WAATHIRIKA WA MABOMU ARUSHA WANENA

Zilikuwa siku, wiki, miezi na sasa ni zaidi ya mwaka umepita tangu
kutokea kwa mlipuko wa bomu kwenye Kanisa la Olasiti, (Parokia ya
Mtakatifu Joseph Mfanyakazi jijini Arusha na kusababisha vifo vya watu
watatu na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Hata hivyo, hadi sasa hakuna kikundi wala mtu yeyote aliyekamatwa na
kufikishwa mahakamani kuhusiana na tukio hili lililoua watu watatu na
kujeruhi wengine zaidi ya 80.

Elizaberth Isidori (20), mmoja wa manusura katika tukio hilo,
amejikuta akilazimika kurudia tena masomo ya kidato cha tatu akiwa
katika Shule ya Sekondari Olasiti. Hiyo ni baada ya bomu kumlipua mguu
wa kulia ambao umekatwa na kumuacha akiwa na ulemavu wa kudumu
maishani mwake.

"Naumia sana nikisikia (Polisi) bado hawajafanikiwa kumkamata mtu wala
kikundi cha watu waliohusika na tukio hili. Pia najisikia vibaya kila
ninaposikia kuna matukio mengine ya ulipuaji yakitokea hapa Arusha
huku wahusika wakifanikiwa kukwepa mkono mrefu wa serikali....
nawaombea (Polisi) ili jitihada zao zizae matunda na wote walionipa
ulemavu huu na kusababisha vifo vya watu wengine wasio na hatia
wakamatwe na kuchukuliwa hatua zinazostahili," ndivyo anavyoanza
kusimulia Elizaberth, mmoja wa majeruhi walioumia vibaya kutokana na
tukio hilo lililojiri Jumapili ya Mei 4, 2013.

Elizaberth ana kila sababu ya kujawa machungu. Taarifa za kuwapo kwa
matukio mengine zaidi ya milipuko ya mabomu huku pia bado kukiwa
hakuna watu au kikundi kilichokamatwa kuhusiana na tukio
lililomsababishia ulemavu siyo habari njema kwake.

Aidha, rekodi zinaonyesha kuwa mbali na tukio la Olasiti, baadhi ya
matukio ya mabomu mjini Arusha ni pamoja na tukio la Juni 15, 2013,
likihusisha bomu lililorushwa kwenye mkutano wa kufunga kampeni wa
Chadema kwenye viwanja vya Soweto ambapo watu wanne waliripotiwa kufa
na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Aprili 13, 2014, mlipuko mwingine wa bomu ulitokea katika baa ya
Arusha Night Park na kusababisha kifo cha mtu mmoja huku watu wengine
14 wakijeruhiwa; Julai 4 mwaka huu akajeruhiwa Sheikh Sood Ally Sood
wa Msikiti wa Qiblatan uliopo Kilombero jijini hapa alijeruhiwa kwa
bomu la kurushwa kwa mkono wakati akila daku nyumbani kwake.

Tukio la hivi karibuni ni lile lililotokea usiku wa kuamkia Jumatatu
(Julai 8), kwenye mgahawa wa Vama Traditional Indian Cuisine ulioko
eneo la Arusha Gymkhana, karibu na eneo la Mahakam Kuu ambapo watu
nane wamejeruhiwa, akiwamo mmoja aliyekatwa mguu katika Hospitali ya
Rufaa ya Selian.

ILIVYOKUWA
Wakati akizungumza na mwandishi wa NIPASHE katika mahojiano maalum
mwishoni mwa wiki kwenye Mtaa wa Mji Mpya uliopo Olasiti, Elizaberth
alisema kuwa anakumbuka vyema juu ya kile kilichotokea Siku hiyo,
Elizaberth alikuwa ni miongoni mwa waumini waliokuwapo katika viunga
vya Kanisa la Olasiti kwa ajili ya maadhimisho ya Ibada ya Misa
Takatifu ya uzinduzi wa jengo la kanisa hilo; ibada iliyokuwa
ikiongozwa na Balozi wa Vatican nchini, Askofu Mkuu, Francis Padilla,
akishirikiana na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha,
Josephat Lebulu.

Elizaberth anasema kuwa siku hiyo alienda kanisani akiwa na wadogo
zake wawili na kukuta waumini wengine kadhaa wakiwa tayari
wameshaingia ndani ya uzio wa kanisa.

"Tulifika katika wakati ambao Askofu Mkuu Lebulu alikuwa anabariki
maji ili Balozi wa Vatican nchini (Askofu Padilla), akate utepe
kuashiria uzinduzi wa jengo la kanisa," anasema Elizaberth.

"Wakati anabariki, mara kuna kitu kama jiwe hivi kikarushwa. Hatukujua
ni nini. Baadhi walidhani ni jiwe limerushwa na kuna mama mmoja
niliyekuwa naye jirani aligongwa na kitu hicho begani kabla hakijatua
chini.

"Ghafla tulisikia mlipuko mkubwa sana... na mimi nikajikuta nipo
chini. Watu walianza kukimbia ovyo. Na mimi nilitaka kukimbia, lakini
nikahisi mguu wangu umekufa ganzi. Sikuweza kabisa.

Nikajitajidi na kujiburuza hadi nje ya uzio. Halafu nikachukuliwa
kwenye gari na kukimbiziwa Hospitali ya Mount Meru," anasema."Kufika
hospitali, nikapelekwa chumba cha upasuaji. Baada ya hapo nikapoteza
fahamu, sikuweza tena kujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea."

Elizaberth anasema kuwa ndugu zake wawili walisalimika, lakini baada
ya hapo yeye alilazwa Mount Meru kwa siku nne. Halafu akahamishiwa
katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC iliyopo mjini Moshi ambako alilazwa
kwa zaidi ya miezi miwili na huko ndiko alikokatwa mguu wake aliokuwa
akiuhisi ganzi kabla ya kubaini baadaye kuwa umeumia vibaya sana.

"Nilienda Aprili 9 na kuruhusiwa kutoka hospitali Juni 27, 2013,"
anasema.Baba mdogo wa Elizabeth anayeishi naye jijini hapa, Edmund
Gaspar Balaga, ambaye ni fundi ujenzi, anasema analishukuru Kanisa la
Olasiti kwa msaada mkubwa iliowapatia wakati wa kumuuguza binti yake,
ikiwa ni pamoja na kumnunulia mguu wa bandia uliogharimu Sh. milioni
mbili.

"Baada ya kupona, tulimhamisha kutoka Shule ya Oljoro kumleta hapa
Olasiti ambako ni jirani na tunakoishi," alisema Balaga.

MWALIMU MONICA
Athari kwa watu waliokumbwa na mlipuko wa bomu Olasiti ni kubwa. Mbali
na Elizaberth ambaye sasa anaishi na mguu wa bandia, mwingine
aliyejeruhiwa vibaya alikuwa ni Monica Tarimo 'Mwalimu Fatuma' (40),
ambaye hadi sasa anaishi na vipande viwili vya vyuma vilivyotokana na
bomu hilo; kimoja kikiwa kimejikita katika sehemu ya mapafu, jirani na
moyo na kingine jirani na pingili za shingo.

Anasema madaktari wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) ambako
alihamishiwa kwa matibabu zaidi kutoka Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya
Mount Meru wameshindwa kuviondoa vyuma hivyo kwavile vimekaa katika
maeneo hatari ya mwili.

Akisimulia kilichotokea siku ya tukio, Mwalimu Fatuma anasema aliona
kitu chenye umbile la yai, kikiwa na nyaya za rangi ya kijani na njano
na kilianguka umbali kama wa mita mbili tu kutoka katika mahala
alipokuwa amesimama.

"Ghafla nikasikia mlipuko mkubwa na nikapata joto kali sehemu ya mguu
wangu wa kulia. Nikanyanyuliwa kwa nguvu na kudondoka chini...
nilishindwa kukimbia kwa sababu kifua kilikuwa kimejaa moshi.

"Baadaye nikaanza kuomba msaada. Watu wakaja kuninyanyua na mimi na
majeruhi wengine kadhaa tukapelekwa katika Hospitali ya Father Babu.
Huko nilishonwa mguu, kidole cha pete na sehemu ya chini ya kidevu,"
anasema.

Anasema baadaye ilipobainika kuwa hali yake inazidi kuwa mbaya,
akahamishiwa katika Hospitali ya Mount Meru na baadaye akasafirishwa
kwa ndege iliyogharimiwa na serikali hadi Muhimbili jijini Dar es
Salaam.

"Hali yangu ilikuwa mbaya kiasi kwamba ilidhaniwa kuwa nimefariki,"
anaeleza.Akiwa hospitali ya mkoa, madaktari walimtoa kipande kimoja
cha chuma kilichokuwa kwenye mapafu lakini walishindwa kutoa kingine
kilichokuwa jirani na moyo na jirani na pingili za shingo.

"Nililazwa Muhimbili kuanzia Mei 8, 2013 hadi Juni 19, 2013."

Anasema baada ya hapo amekuwa akiendelea na shughuli zake za
kufundisha, lakini kila mara akihudhuria kliniki kuangalia maendeleo
yake ya afya yake.

"Hadi sasa nimeshakwenda kliniki mara tatu, yaani Agosti na Novemba
mwaka jana na pia Mei mwaka huu. Nimeelezwa kila ninapojisikia vibaya
naweza kwenda tena," anasema.

Mbali na kupata majeraha makubwa, Mwalimu Fatuma anasema vilevile kuwa
ameathiriwa sana kisaikolojia na matokeo yake, kila mara anaposikia
mshindo hukumbukia tukio la mabomu Olasiti na kukosa raha.

"Sikutegemea tukio kama lile litokee kanisani au sehemu nyingine ya
mkusanyiko wa watu. Inasikikitisha sana kutokea kwa mambo haya (ya
mabomu) ya kinyama," anasema Mwalimu Fatuma, ambaye analishukuru
kanisa la Olasiti, serikali, madaktari na watu wote waliomsadia katika
kupigania maisha yake.
Naye anaiomba serikali iliwezeshe Jeshi la Polisi kwa hali na mali ili
kuhakikisha kwamba linapata nguvu na uwezo wa kuwakamata watu wote
wanaojihusisha na matendo ya kinyama kama hayo ya kulipua mabomu
kwenye hadhara ya watu wasiokuwa na hatia.

KAULI YA POLISI
Akizungumzia matukio ya mabomu ya Arusha, Mkurugenzi wa Upelelezi wa
Makosa ya Jinai (DCI) wa Jeshi la Polisi nchini, Isaya Mngulu,
amekaririwa akisema kuwa hayana uhusiano na matukio ya kigaidi
yanayofanywa nchini Kenya; ambako kumekuwa na mashambulizi ya ya
kigaidi ya kundi la Al Shabaab.

"Matukio ya mabomu Arusha hayana uhusiano na matukio kikagidi kama
yanayotokea nchini Kenya. Pia hayana uhusiano na masuala ya kisiasa,"
alisema Mngulu.

Alisema uchunguzi uliofanywa na Polisi umebaini kuwapo kwa kikundi
kinachojihusisha na matukio hayo na kwamba, jeshi hilo litahakikisha
watuhumiwa wote wanasakwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ili kufanikisha
kukamatwa kwa watuhumiwa wa matukio hayo kwani suala la ulinzi na
usalama ni jukumu la kila mwananachi.

Aidha, watuhumiwa 16 wanaodaiwa kuhusika na matukio ya ulipuaji wa
mabomu walipandishwa kizimbani wiki iliyopita katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Arusha na kunyimwa dhamana.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, watuhumiwa wanadaiwa kulipua mabomu
kati ya mwaka 2010 hadi Februari, mwaka huu, maeneo mbalimbali nchini,
kinyume cha kifungu cha 118 (1) (a) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya
mwaka 2002.
CHANZO: NIPASHE Na John Ngunge

0 Comments:

Post a Comment