RAIS, Jakaya Kikwete anatazamiwa kufungua mkutano wa 45 wa Umoja wa Mabunge ya jumuiya ya Madola, (CPA), Kanda ya Afrika ambao unajuisha wajumbe 500 kutoka nchi 17 wanachama.
Aidha,miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa na mkutano huo ni endapo chaguzi za ukanda huo kama ni huru na haki na sababu zinazopelekea kutokea ugomvi mara zinapomalizika.
Pia wataangalia sababu ya uchumi wa nchi hizo kuonekana kukua kwa kasi huku hali halisi ya wananchi wake ikiendelea kuwa duni kiasi cha baadhi ya wananchi kwenye nchi kufa kwa kukosa chakula.
Hayo yalisemwa jana na Spika wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda, ambaye pia ni Rais wa CPA Kanda ya Afrika alipokuwa akiongea na waandishi wa habari jijini hapa juu ya mkutano huo utakaofunguliwa rasmi julai 24, mwaka huu ingawa vikao mbalimbali ya kiutendaji vimeanza kuanzia jana.
Alisema kuwa chombo hicho hufanya mkutano wake mara moja kwa mwaka ambapo nchi inayojitolea kuandaa mkutano wa mwaka unaofuata hupewa fursa ya kukiongoza kwa mwaka mmoja ambapo baada ya Tanzania, spika wa bunge la Lesotho, Sephiro Motanyane atakabidhiwa rasmi uongozi wa chombo hicho.
Alisema kuwa wanatarajia kujadili changamoto zinazozikabili hizo ambapo katika hatua ya awali watakaa kulingana kanda wanazotoka kwa kile alichoeleza kuwa kila eneo linachangamoto zake ambapo baadaye watakuja kuyawasilisha kwenye mkutano wa pamoja.
"Nchi zetu (wanachama wa CPA) zinakua kiuchumi, lakini zote bila kubagua wanachi wake bado wana hali duni, wanakabiliwa na njaa, utapia mlo, vita. Dalili ya kukua, uchumi unaonekana unapaa kitakwimu, lakini mbona watu wetu wana njaa? Tunataka kushirikiana kumaliza haya.
"Tunataka kujadili kuona chaguzi zetu ni huru kama tunavyotaka, maana ukimalizika uchaguzi, magomvi yanaanza, je ni kanuni zetu hazifuatwi au tatizo ni nini," alisema Spika, Makinda.
Alisema kuwa pia wataangalia tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana ambapo mjadala huo utawahusisha watoa mada kutoka bunge lao la vijana ambalo lina muhula watatu sasa toka lianzishwe.
Spika Makinda alisema kuwa kwa miaka 10 sasa Tanzania inaongoza sekretarieti ya CPA baada ya Zimbabwe kujiondoa kwenye umoja huo ambapo wanatazamia kujenga makao makuu na kitega uchumi eneo la Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo wa siku saba kuanzia julai 20 mpaka 26, mwaka huu mbali na maspika utawashirikisha waangalizi na watumishi kutoka mabunge wanachama ambapo kauli mbiu yake ni umuhimu wan chi za jumuiya ya madola katika kukabiliana na changamoto za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Katika hatua nyingine, Spika Makinda aliseka kuwa alikuwa amewatuma wabunge watano wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwenda Australia kuhudhuria mkutano wa wa 20 wa kimataifa wa kupambana na ukimwi lakini hajui kama mkutano huo utaendelea.
Alisema kuwa hiyo inatokana wajumbe wa jumuiya ya kimataifa ya kupambana na maradhi ya ukimwi, zaidi ya 100 kufariki wakati waliokuwa wakienda kwenye mkutano huo baada ya ndege waliyokuwa wakisafiria ya shirika la ndege la Malaysia namba MH17 kuanguka katika eneo la vita nchini Ukraine katika uwanja wa kuala Lumpur julai 18, mwaka huu.
0 Comments:
Post a Comment