Saturday, October 13, 2012

PPF YATUMIA BILIONI 561 KUSOMESHA WATOTO WALIOFIWA NA WAZAZI WAO


MFUKO wa hifadhi za jamii wa PPF umetumia zaidi ya shilingi milioni 561 kwa ajili ya kulipia ada na gharama za masomo  ya elimu ya sekondari kwa watoto 1,095 ambao wazazi wao walifariki wakiwa wanachama wa mfuko huo.

Hayo yalisemwa Oktoba 10,mwaka huu na Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo, Willium Erio alipokuwa akitoa taarifa ya utendaji kwa wajumbe wa mkutano wa 22 wa PPF unaoendelea kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha jijini Arusha, (AICC).

Alisema kuwa fedha hizo zililipwa kwa ajili ya mwaka 2011 ambapo alisema kuwa watoto wanaonufaika na  fao hilo la elimu ni wale ambao wazazi wao walikuwa wanachama waliwasilisha michango yao angalau kwa miaka mitatu.

Erio alisema kuwa PPF walianza kutoa fao hilo kuanzia mwaka 2003 kwa lengo la kuwawezesha watoto wa wanachama ambao wamefariki kuweza kuendelea na masomo ya sekondari ambapo kwa sasa wanaangali uwezekano wa kuwasomesha mpaka kidato cha tano na sita kwa wale watakaokuwa wamefanya vizuri katika mitihani yao ya mwisho ya kidato cha nne.

Mkurugenzi mkuu huyo wa PPF alisema kuwa mfuko huo umeendelea kuboresha huduma zake ikiwa ni pamoja na kutoa mikopo kwa wanachama kupitia vya kuweka na kukopa (SACCOS) vilivyopo katika maeneo ya kazi ambapo mpaka kufikia juni mwaka huu jumla ya shilingi bilioni 45.4 zimetolewa kwa SACCOS 36.

Erio alisema mfuko huo unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ile ya waajiri kukwepa kuwaandikisha wafanyakazi wao kwenye mfuko kwa kuwaajiri kwa muda mfupi ambapo wengine huajiriwa lakini huendelea kulipwa kwa kutwa ambapo hali hiyo alidai hujitokeza zaidi kwenye mashamba makubwa na viwanda vya usindikaji.

Aidha aliwataka wanachama kuwa wanaandika wosia ili kurahisha na kuharakisha utoaji wa mafao kwa wasimamizi wa miradhi au wategemezi pale inapotokea mwanachama kafariki akiwa katika ajira jambo alilosema kuwa pia litasaidia kuondoa malumbano ya miradhi ambayo imekuwa kero kwa wajane na watoto wa marehemu.

Erio alisema kuwa wameongeza wigo wa uwekezaji ambapo kwa sasa wapo kwenye maandalizi ya mwisho kwa ajili ya kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya ofisi na biashara mkoani Arusha kwani tayari michoro imeshakamilika ambapo mchakato unaendelea kwenye mikoa ya dare s Salaam na Mtwara.




No comments:

Post a Comment