MWENYEKITI wa Taifa wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA) amesema kuwa vuguvugu la mabadiliko (M4C) hapa nchini haliwezi kumalizwa kwa jeshi la polisi kutumia risasi kutisha na kuua wananchi bali kwa serikali kutenda haki.
Aidha amelitaka Jeshi la Polisi nchini kufanya shughuli zake kwa utaalamu kwa kuzingatia sheria na kanuni zinazolisimamia na kuepuka kutumiwa kutekeleza matakwa ya watawala wanaowaagiza kuwanyanyasa wapinzani.
Aliyasema hayo Oktoba 10, mwaka huu kwenye mtaa wa Jamhuri wakati akimnadi mgombea udiwani wa chama hicho kwenye kata ya daraja Mbili, Prosper Msofe ambaye hata hivyo hakuweza kuhudhuria mkutano huo kwani alikuwa amelazwa hospitali ya mkoa ya Mount Meru akipatiwa matibabu ya uti wa mgongo baada ya kushikiliwa na jeshi la polisi kituo cha kati kwa usiku mmoja.
Mbowe mbali ya kumuombea kura mgombea huyo alimtaka kutotishika kwa tukio lililompata badala yake iwe changamoto ya kuzidi kudai na kupigania haki kwa maslahi ya umma huku akiongeza kuwa kama sababu ya Chadema kuitwa chama cha vurugu ni kwa kitendo chake cha kuwahamasisha watu kudai na kupigania haki zao basi acha kiendelee kutambulika hivyo.
Alielezea kushangazwa na hatua ya Tume ya Usimamizi ya Uchaguzi nchini kushindwa kutangaza uchaguzi wa kata nne za jiji la Arusha ambazo zilikuwa zinaongozwa na madiwani wa waliotimuliwa Chadema toka mwaka jana licha ya juhudi mbalimbali walizofanya ikiwemo kuikumbusha tume hiyo kwa kuiandikia barua.
Kata hizo ni ile ya Elerai, Kimandolu, Kaloleni, Themi na ile ya Sombetini iliyokuwa ikishikiliwa na Chama Cha Mapinduzi kupitia diwani Alphonce Mawazo ambaye alijivua gamba kwa kutoka CCM na kujiunga na Chadema.
“Woga wao wanajua nguvu ya Chadema kwa sasa, wanaogopa kuona Chadema tukishinda viti hivi na kuingiza madiwani sita pamoja na wa viti maalum idadi ya madiwani wetu itakuwa kubwa hivyo tutaongoza Halmashauri ya jiji la Arusha” alisema Mbowe huku akisistiza kuwa dhuluma ina mwisho.
Akiongelea suala la utaratibu wa chama hicho kuwachangisha wanachama wake fedha kwenye mikutano yao kwa ajili ya kuchangia gharama za uendeshaji mbunge huyo wa Hai alisema kuwa Chadema inajengwa na watu wenye fedha safi kama hizo kama ambavyo baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alivyokusanya fedha kwa ajili ya kutafuta uhuru na kuwa hawaitaji fedha za mafisadi.
Kwa upande wake aliyekuwa mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema aliwataka polisi wadogo kutokubali kutumiwa kutekeleza amri za kikandamizaji za viongozi wao kuumiza wananchi kwani mwisho wa siku watakaohukumiwa ni wao huku akitolea mfano wa tukio la Iringa ambalo polisi wa cheo cha chini ndiye aliyefikishwa mahakamani huku kiongozi wake akiendelea na kazi kama kawaida.
Alisema kuwa kwenye vurugu za Arusha za januari 5, mwaka jana walikufa watu watatu ambapo polisi wa vyeo vya juu ndiyo walioongezewa vyeo huku wale wa chini wakiambulia patupu.
No comments:
Post a Comment