MGOMBEA udiwani kata ya Daraja Mbili kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), Prosper Msofe amelazwa kwenye hospitali ya mkoa ya Mount Meru akisumbuliwa na maumivu ya uti wa mgongo baada ya kuzuiliwa kwenye kituo cha polisi cha kati, Arusha usiku wa Oktoba 8, Mwaka huu.
Katibu wa wilaya ya Arusha wa Chadema, Martin Sarungi na aliyekuwa mbunge wa Arusha, Godbless Lema waliwaeleza waandishi wa habari mbele ya kituo cha polisi kuwa mgombea wao alikamatwa majira ya saa mbili usiku eneo la Friends Corner baada ya kuhoji sababu wamachinga kunyang’anywa bidhaa zao na Ramadhani Kalamba (56) anayedai kuwa Halmashauri ya jiji imempa jukumu la kuwaondoa machinga katikati ya jiji.
“ Msofe alihoji sababu za Ramadhani kuchukua mali za machinga majira ya usiku wakati ambao halmashauri haifanyi kazi alikuwa akizipeleka wapi na ni nani aliyempa mamlaka ya kuchukua vitu hivyo ndipo gari la polisi likafika na kumchukua” alisema Lema.
Walisema kuwa baada ya kupata taarifa za mgombea wao huyo kukamatwa baadhi ya wanachama na viongozi walimfuatilia mpaka kituo cha polisi kwa lengo la kumwekea dhamana jambo ambalo lilishindikana ndipo majira ya saa nne usiku wakaamua kuondoka.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi mkoani hapa,(RPC), Liberatus Sabas alikanusha madai hayo kwa kile alichoeleza kuwa mgombea huyo hakunyimwa bali alikataa dhamana mwenyewe ambapo alidai kuwa alikamatwa na askari wa doria na kufikishwa polisi kwa tuhuma za kumpiga ngumi ya kifuani Kalamba.
Alisema kuwa jeshi la polisi walipata taarifa kuwa Kalamba anashambuliwa ndipo askari wa doria walipofika na kumchukua Msofe ambapo alisema kuwa mzozo baina ya wawili hao ulitokana na hatua ya Msofe kuhoji sababu za Kalamba kutaka wamichinga hao waondoke eneo hilo huku akijaribu kumzuia asiendelee kutangaza.
Awali jana majira ya saa nne asubuhi mgombea huyo wa Chadema alienda kupatiwa matibabu kwenye zahanati ya polisi akiwa chini ya ulinzi mkali wa jeshi la polisi ambapo daktari wa zahanati hiyo alishauri apelekwe hospitali ya mkoa kwa uchunguzi zaidi lakini polisi waliamua kumpeleka mahakama ya mwanzo ya maromboso.
Baadhi ya viongozi wa Chadema waliokuwa mahakamani hapo walikwenda kuuona uongozi wa mahakama na kuwaonyesha cheti alichopatiwa mtuhumiwa huyo kinachomtaka apelekwe hospitali ya mkoa kwa uchunguzi zaidi jambo ambalo linadaiwa pengine ndilo lililopelekea mtuhumiwa huyo kutofikishwa mbele ya hakimu.
Mgombea huyo ambaye alikuwa amepakiwa kwenye gari ya polisi yenye namba za usajili PT 1844 ambayo ubavuni imeandikwa OCD Arusha alikaa rumande ya mahakama hiyo kwa zaidi ya saa moja ambapo gari hilo lilirudi likiwa limeongeza idadi ya askari wenye silaha wakiongozwa na Mkuu wa Polisi wa wilaya hii (OCD), G A Muroto na kumchukua ambapo walimpeleka moja kwa moja hospitali ya mkoa ya Mount Meru.
Baada ya kumuona daktari mgombea huyo ambaye polisi walizuia waandishi kuzungumza naye alilazwa hospitalini hapo kwenye wodi namba moja ambayo ni ya upasuaji na majerehi akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi.
Kuanzia asubuhi wananchi wengi walijitokeza kwenye kituo cha polisi cha kati ambapo walikuwa wakikimbia kwa miguu wengine kwa magari na pikipiki kufuatilia hatua kwa hatua eneo mgombea huyo alipokuwa akipelekwa ambapo shughuli za mahakama ya mwanzo Maromboso zilisimama kwa muda wakati mtuhumiwa huyo alipokuwa akiingia na akiondolewa ambapo kwenye hospitali ya Mount Meru wananchi wengi walisimama eneo la mapokezi huku wakipewa taarifa ya kile kinachoendelea na viongozi wa Chadema.
Wagombea wengine katika kinyang’anyiro hicho na vyama vyao kwenye mabano ni Philip Philip, (CCM), Mohamed Msuya (NCCR-Mageuzi), Willium Laizer, (TLP) na Zani Zakaria, (CUF).
No comments:
Post a Comment