SHIRIKA la Hifadhi za Taifa nchini, (TANAPA) limeandaa tuzo maalum kwa waandishi wa habari nchini wanaoandika habari bora na nzuri kwa ajili ya kuhamasisha utalii wa ndani na umuhimu wa uhifadhi endelevu ambapo washindi wa sita wa kwanza mbali ya zawadi ya fedha taslimu, tuzo na cheti watapata fursa ya kutembelea moja ya nchi za Jumuiya ya Uchumi Kusini mwa Africa(SADC) .
Meneja uhusiano wa shirika hilo, Pascal Shelutete aliwaeleza wandishi wa habari hayo Oktoba 6, mwaka huu kwenye makao makuu ya shirika hilo yaliko jijini Arusha kuwa shindano hilo litajumuisha makala zilizotoka magazetini, vipindi vilivyoandaliwa radioni na kwenye luninga vilivyofanyika kuanzia Januari mosi mpaka Desemba 31, 2012.
Alisema kuwa kwenye shindano hilo linalotarajiwa kufanyika kwa uwazi mkubwa litawashirikisha waandishi wote hapa nchini wanaofanya kazi kwenye magazeti, radio na luninga ambapo washindi wa kwanza kwenye kila kundi atapata fedha taslimu shilingi milioni 1.5, cheti, ngao na safari ya mafunzo ya zaidi ya siku saba kwenye moja ya nchi za SADC ambayo hakuitaja kwa ajili ya kujifunza masuala ya utalii wa ndani.
Shelutete alisema kuwa washindi wa pili watapata fedha taslim shilingi milioni moja na ngao wakati washindi watatu watapata fedha taslim shilingi laki 5 na cheti ambapo washindi 18 wanatarajiwa kupatikana 9 kwenye habari za uhifadhi na tisa wengine kwenye uhifadhi wa utalii wa ndani.
Alisema kuwa TANAPA imeamua kutoa tuzi hizo ili kuongeza hamasa kwa waandishi kuandika habari za zitakazowahamasisha wananchi kutembelea vivutio vilivyopo hapa nchini ili kukuza utalii wa ndani kwani kwa sasa wanaoongoza kwa kutembelea hifadhi ni watalii kutoka nje ya nchi.
Shelutete alisema kuwa pia shindano hilo limelenga kutoa elimu zaidi kwa wananchi kupitia vyombo vya habari kuona umuhimu wa kulinda na kuhifadhi maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kuhifadhiwa kwa kuepuka kuyavamia au kuingiza mifugo kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.
Alisema kuwa wanaotaka kushiriki shindano hilo wanaweza kutembelea mtandao wa shirika hilo www.tanzaniaparks.com na kujaza fomu maalum kisha wataituma kwa mkurugenzi mkuu wa TANAPA kupitia meneja uhusiano.
No comments:
Post a Comment