VYAMA 14 VYA SIASA KUANZA KUCHUKUA FOMU ZA UTEUZI WA WAGOMBEA WA URAIS AGOSTI 9




Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza ratiba ya kuchukua fomu za uteuzi kwa wagombea wa nafasi za Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ambapo jumla ya vyama 14 vya siasa vimewasilisha ratiba zao. Zoezi hilo litaanza kesho, tarehe 9 Agosti 2025, na kuendelea hadi tarehe 27 Agosti 2025.

Akizungumza leo tarehe 8 Agosti 2025 jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima, amesema:

"Hadi leo tarehe 08 Agosti, 2025, tumepokea barua kutoka katika vyama vya siasa kumi na nne (14) zikiainisha tarehe na muda ambao wanachama wa vyama vyao waliowapendekeza kugombea nafasi za Kiti cha Rais na Makamu wa Rais watafika ofisi za Tume zilizopo Njedengwa Jijini Dodoma kwa ajili ya kuchukua Fomu za Uteuzi."

Kwa mujibu wa Kailima, vyama vitakavyoanza kuchukua fomu kesho tarehe 9 Agosti 2025 ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), National Reconstruction Alliance (NRA), na Alliance for African Farmers Party (AAFP).

Ratiba ya vyama vingine na tarehe za kuchukua fomu ni kama ifuatavyo:

  • Chama cha MAKINI – 10 Agosti 2025

  • The National League for Democracy (NLD) – 10 Agosti 2025

  • United Peoples’ Democratic Party (UPDP) – 10 Agosti 2025

  • African Democratic Alliance Party (ADA–TADEA) – 11 Agosti 2025

  • Union for Multiparty Democracy (UMD) – 11 Agosti 2025

  • Tanzania Labour Party (TLP) – 11 Agosti 2025

  • Chama Cha Kijamii (CCK) – 12 Agosti 2025

  • Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) – 12 Agosti 2025

  • Alliance for Democratic Change (ADC) – 12 Agosti 2025

  • Democratic Party (DP) – 13 Agosti 2025

  • National Convention for Construction and Reform (NCCR–MAGEUZI) – 15 Agosti 2025

Kailima amesema tayari Tume imewaandikia barua vyama hivyo kuwajulisha ratiba husika.

"Aidha, ni muhimu tukumbuke kuwa, ratiba hii inahusu vyama kumi na nne (14) pekee vilivyowasilisha taarifa hadi kufikia leo tarehe 08 Agosti, 2025, hivyo iwapo vyama vingine vitajitokeza, tutaandaa ratiba husika na kuwajulisha."

Amewapongeza wadau wa siasa kwa maandalizi yao ya uchaguzi.

"Ninavipongeza vyama vyote vya siasa kwa kuendelea kufanya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, na Tume kwa upande wake itazingatia katiba, sheria na kanuni wakati wote wa mchakato wa uchaguzi."


0 Comments:

Post a Comment