Chama cha ACT-Wazalendo kimetangaza kwa mara ya kwanza wagombea wake wa nafasi za juu za uongozi kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, kupitia Mkutano Mkuu wa Taifa uliofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na wajumbe kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani, chama hicho kimemuidhinisha Othman Masoud Othman kuwa mgombea wa urais wa Zanzibar, huku Luhaga Mpina akiteuliwa rasmi kuwa mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Matokeo Rasmi ya Uchaguzi wa Ndani ya Chama
Akisoma matokeo ya uchaguzi huo mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu, Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Uchaguzi ya ACT-Wazalendo, Mbarala Maharagande, alisema:
"Kwa nafasi ya urais wa Zanzibar, jumla ya kura zilizopigwa ni 610. Ndugu Othman Masoud amepata kura 606, sawa na asilimia 99.5. Kura tatu zilikuwa za hapana, na kura moja imeharibika."
Kuhusu nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Maharagande alifafanua kuwa:
"Ndugu Luhaga Mpina amepata kura 559 kati ya kura halali 605, sawa na asilimia 93, akimshinda mpinzani wake Ndugu Aaron Kalikawe aliyepata kura 46, sawa na asilimia 7.7. Kura tatu kati ya zote zilizopigwa ziliharibika."
Fatma Fereji Ateuliwa Mgombea Mwenza
Mara baada ya kutangazwa mshindi, Luhaga Mpina aliteua jina la Fatma Abdulhabib Fereji kuwa mgombea mwenza wake kwa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akizingatia masharti ya Ibara ya 68, kifungu kidogo cha kwanza (a) ya Katiba ya ACT-Wazalendo. Halmashauri Kuu ya chama hicho iliridhia uteuzi huo bila upinzani.
Kauli za Viongozi Baada ya Uteuzi
Akitoa salamu za shukrani mbele ya wajumbe, Othman Masoud alisema:
"Chama kimenipa heshima kubwa ya kusimamia matarajio ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla. Nitajitahidi kwa dhati kutimiza wajibu huu kwa moyo wa uadilifu na uwajibikaji."
Aliendelea kueleza kuwa licha ya Tanzania kuwa nchi tajiri kwa rasilimali, wananchi wengi wanaendelea kuishi katika hali ya umasikini kwa sababu ya kasoro katika mifumo ya uongozi.
"Rasilimali za taifa zimegeuzwa kuwa kama keki inayogawiwa kwa wachache. Mfumo huu wa sasa wa utawala hautupeleki mbali. Tunahitaji mageuzi ya kweli yenye msingi wa uwajibikaji wa kisiasa," alisisitiza.
Kwa upande wake, Luhaga Mpina, ambaye ni mwanasiasa mkongwe aliyejiunga na ACT-Wazalendo akitokea CCM, alisema:
"Nawashukuru wajumbe wa mkutano huu kwa imani kubwa mliyonipa. Nitashirikiana na viongozi wa chama na wananchi kuhakikisha ujumbe wa mageuzi unafika kila pembe ya nchi."
Aliwahimiza wanachama na wafuasi wa ACT-Wazalendo kuanza maandalizi ya kampeni kwa bidii akisema:
"Kampeni zinaanza hivi karibuni. Tutaanza kazi saa sita usiku kampeni zikianza rasmi, tukizunguka mikoa yote kuwasilisha ujumbe wa matumaini, mabadiliko na Tanzania mpya."
Mpina aliongeza kuwa uamuzi wake wa kujiunga na ACT-Wazalendo ulikuwa wa muda mrefu lakini wenye matumaini makubwa:
"Nimechelewa kujiunga, lakini sijaikosa nafasi ya kushiriki katika mageuzi ya kweli. ACT ni chama kinachosimamia misingi ya demokrasia, uwazi na haki."
Uchaguzi Mkuu wa 2025 Wazidi Kusogea
Tanzania inajiandaa kwa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba 2025, ambapo wananchi watawachagua viongozi kuanzia ngazi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, Rais wa Zanzibar, Wabunge, Wawakilishi, hadi Madiwani.
Kwa hatua hii ya uteuzi wa wagombea wake, ACT-Wazalendo imeonesha dhamira yake ya kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi huo, kwa kaulimbiu ya kuleta mageuzi ya kweli katika mfumo wa uongozi na maisha ya wananchi wa Tanzania.


0 Comments:
Post a Comment