Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limepanga kujenga minara 1,400 ya mawasiliano katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 na 2025/2026 ili kuimarisha huduma za mawasiliano hususan vijijini,
Aidha, Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango, amezindua rasmi dashboard kuu ya usimamizi wa mashirika ya umma jijini Arusha.
Akizungumza kwenye banda la Maonesho la TTCL kando ya kikao kazi cha tatu cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Mashirika na Taasisi za Umma, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, alisema mpango huo wa ujenzi wa minara ni sehemu ya utekelezaji wa dira ya serikali kuelekea uchumi wa kidijitali.
“TTCL peke yetu ndiyo wamiliki wa mkongo wa taifa ambao serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa. Lengo ni kuhakikisha tunawafikishia wananchi wote nchini mawasiliano yenye kasi kubwa na ya uhakika,” alisema Marwa.
Alifafanua kuwa kwa mwaka huu minara 626 inajengwa ambapo zaidi ya minara 100 imekamilika ndani ya miezi sita tangu ujenzi uanze.
“Hadi Juni 2026 minara yote 626 itakuwa imekamilika. Kisha utekelezaji wa ujenzi wa minara 850 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 utaanza mara moja. Na sisi, kwa kuwa tuna huduma ya mkongo, minara hii yote tutaunganisha moja kwa moja na mkongo wa taifa ili kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata mawasiliano yenye kasi zaidi,” alisisitiza.
Aidha, Marwa alieleza kuwa TTCL imewekeza pia katika huduma za kituo cha kuhifadhi taarifa (data centre) na miundombinu ya kimkakati, hatua inayokwenda sambamba na uzinduzi wa dashboard mpya ya usimamizi wa mashirika ya umma.
“Anachofanya Ofisi ya Msajili wa Hazina kupitia dashboard hii kimsingi kinategemea mawasiliano. Hivyo jukumu la TTCL ni kuhakikisha miundombinu hiyo inafanya kazi kwa ufanisi ili kusaidia serikali kufanikisha mpango wake wa kidijitali,” aliongeza.
Katika kikao hicho, Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango, alizindua rasmi dashboard kuu ya usimamizi wa mashirika ya umma ambayo ni sehemu ya mfumo wa Public Investment Management System (PIMS).
“Dashboard hii itasaidia kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika usimamizi wa mashirika ya umma nchini. Ni hatua muhimu ya kulinda uwekezaji wa umma na kuimarisha ufuatiliaji wa utendaji wa mashirika haya,” alisema Dkt. Mpango.
Awali, Kaimu Mkurugenzi wa TEHAMA katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, Donald Samwel Juma, alimweleza Makamu wa Rais kuwa mfumo huo umejengwa kwa madirisha makuu matatu:
Kwa mujibu wa Juma, dashboard hiyo imetengenezwa kutoa taarifa kwa wakati na kwa urahisi wa uelewa ili kusaidia watoa maamuzi wa ngazi za juu wakiwemo Msajili wa Hazina na viongozi wakuu wa serikali.
Alifafanua zaidi kuwa dashboard inahusisha maeneo manne makuu:
Makamu wa Rais alihitimisha kwa kuwataka viongozi wa mashirika ya umma kutumia dashboard hiyo kikamilifu ili kuongeza ufanisi, kuondoa urasimu na kuhakikisha huduma kwa wananchi zinaboreshwa.
“Serikali imewekeza katika mifumo hii ya kidijitali kwa lengo la kuimarisha ufanisi na kuongeza tija. Ni wajibu wa kila shirika kuhakikisha linafanya kazi kwa weledi na matokeo chanya,” alisema Dkt. Mpango.
Mipango ya TTCL sambamba na uzinduzi wa dashboard inaonesha dhamira ya serikali na taasisi zake kuhakikisha Tanzania inasonga mbele kuelekea uchumi wa kidijitali ifikapo mwaka 2050.









No comments:
Post a Comment