Sunday, August 24, 2025

Makamu wa Rais Akabidhi Tuzo kwa Mashirika ya Umma Yaliyoonyesha Ufanisi 2023/2024


ZAIDI ya Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa taasisi na mashirika ya umma 600 wamekutana kwenye Kikao Kazi  jijini Arusha, ambapo mashirika yaliyofanya vizuri katika mwaka wa fedha 2023/2024 yametuzwa kwa kuonyesha utendaji bora na ufanisi wa hali ya juu.



Tuzo hizo zilikabidhiwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, aliyefungua rasmi kikao hicho leo Agosti 24,  2025, kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Kikao hicho kimeandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, kikilenga kuhimiza utawala bora, uwajibikaji, usimamizi thabiti wa mali za umma na kutathmini mchango wa taasisi za umma katika maendeleo ya Taifa.

Serikali Yataka Matokeo Yenye Tija Kutokana na Uwekezaji

Akiwa mgeni rasmi, Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, alisema Serikali imewekeza zaidi ya shilingi trilioni 86.29 katika mashirika ya umma, hivyo ni lazima yaonyeshe matokeo ya moja kwa moja katika maisha ya wananchi.

“Usimamizi madhubuti wa mashirika ya umma ni miongoni mwa ajenda ya serikali ili kuhakikisha uwekezaji mkubwa wa trilioni 86.29 unaleta tija kwa Taifa,” alisema.

Alisisitiza kuwa mageuzi ya taasisi hizo si suala la hiari tena, bali ni wajibu wa msingi kwa watendaji wote, ili kuyafanya mashirika yawe na mchango mkubwa katika ajira, huduma kwa jamii na ukusanyaji wa mapato ya serikali.

Mashirika Yaliyopewa Tuzo

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, alitangaza orodha ya taasisi zilizopokea tuzo hizo kwa mujibu wa makundi na vigezo mbalimbali vya kiutendaji, ikiwemo ukuaji wa mapato, udhibiti wa matumizi, faida halisi, ukwasi, rejesho la uwekezaji na utekelezaji wa hoja za CAG.

Mashirika ya Biashara:

  • Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)

  • Bohari ya Dawa (MSD)

  • Shirika la Madini la Taifa (STAMICO)

  • Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)

  • Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC)

Mashirika Yasiyofanya Biashara:

  • Wakala wa Huduma za Misitu (TFS)

  • Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB)

  • Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)

  • Wakala wa Usajili wa Leseni na Biashara (BRELA)

  • Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Bima (TIRA)

Mashirika ya Utawala Bora (ya biashara na yasiyo ya biashara):

  • Benki Kuu ya Tanzania (BOT)

  • Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA)

  • Soko la Bidhaa Tanzania (TMX)

  • Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA)

  • Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA)

Huduma Bora kwa Jamii:

  • Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)

  • Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi Ghalani (WRRB)

  • Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA)

  • Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA)

  • Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC)

Mapato Yasiyo ya Kodi Yaendelea Kupaa

Dkt. Mpango alibainisha kuwa mapato yasiyo ya kodi kutoka taasisi za umma yameongezeka kwa asilimia 37 katika kipindi cha miaka minne, kutoka shilingi bilioni 753.9 mwaka 2019/2020 hadi shilingi trilioni 1.028 mwaka 2024/2025.

Alisema matarajio ya Serikali kwa mwaka huu wa fedha ni kufikia shilingi trilioni 2, akisisitiza kuwa hilo linawezekana endapo kila taasisi itajipanga kuongeza angalau mara mbili ya kile ilichochangia mwaka uliopita.

“Tunatarajia taasisi ambazo bado hazijaanza kutoa mchango katika mfuko mkuu wa Serikali zifanye tathmini ya kina na zichukue hatua haraka,” alisema.

Taasisi za Umma na Dira ya Taifa 2050

Katika hotuba yake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo, alisisitiza kuwa mashirika ya umma ni watekelezaji wakuu wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Alisema mashirika hayo yanapaswa kuwa chachu ya maendeleo kwa kuboresha huduma, kuunga mkono sekta binafsi, kukuza utafiti na sayansi, pamoja na kujenga rasilimali watu bora.

Mageuzi ya Taasisi Yabeba Matumaini

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, alisema kikao hicho ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kuimarisha usimamizi wa mashirika ya umma, na kuhakikisha yanaendeshwa kwa tija na uwazi.

Alibainisha kuwa hadi sasa mashirika 57 ya kimkakati yamepewa uhuru wa kujiendesha kibiashara, taasisi 14 zimeunganishwa kuwa sita, na taasisi tatu zimeshafutwa baada ya majukumu yake kupitwa na wakati.

Aliongeza kuwa taasisi nyingi zimeboresha uwazi kwa kuchapisha taarifa za fedha, kushiriki vikao vya wazi na vyombo vya habari, na kufanikisha kupungua kwa utegemezi wa ruzuku ya serikali.

“Mapato yasiyo ya kodi kutoka taasisi za umma yameongezeka kwa zaidi ya asilimia 60 tangu mwaka 2020/2021 hadi sasa, hii inaonyesha mageuzi haya yana tija,” alisema.

Kaulimbiu ya Mwaka

Kikao Kazi cha mwaka huu kiliendeshwa chini ya kaulimbiu:
"Kujenga Ushirikiano Endelevu katika Mazingira ya Ushindani Kimataifa – Wajibu wa Mashirika ya Umma."

Kaulimbiu hiyo inalenga kuzihamasisha taasisi kujiimarisha katika ushindani wa kikanda na kimataifa kwa kushirikiana na sekta binafsi, kutumia teknolojia na kuongeza tija katika utoaji wa huduma.


No comments:

Post a Comment