Wakati wa kilele cha Maonesho ya Sikukuu ya Wakulima Nane Nane yanayofanyika katika Viwanja vya Nzuguni, Jijini Dodoma, Manaibu Makatibu Wakuu kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI wametembelea banda la Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na kupongeza juhudi kubwa zinazofanywa na wakala huo katika uboreshaji wa miundombinu ya barabara nchini, hasa maeneo ya wakulima.
Ujumbe huo uliongozwa na Mhandisi Rogatus Mativila (Naibu Katibu Mkuu – Miundombinu), Sospeter Mtwale (Naibu Katibu Mkuu – Utawala na Rasilimali Watu) pamoja na Prof. Tumaini Nagu (Naibu Katibu Mkuu – Afya).
Katika ziara hiyo, walipewa maelezo ya kina kuhusu majukumu ya TARURA, utekelezaji wa miradi ya barabara pamoja na mipango ya maendeleo inayoendelea, yakitolewa na wataalamu wa wakala huo wakiongozwa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano, Catherine Sungura.
TARURA imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa barabara kwa lengo la kuimarisha usafiri na uchukuzi, hasa katika maeneo ya vijijini ambapo kilimo, ufugaji na uvuvi ni shughuli kuu za kiuchumi.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Catherine Sungura, Wakala unaendelea na jitihada za kuongeza mtandao wa barabara unaopitika kwa mwaka mzima na kuwawezesha wananchi kufikia masoko, huduma za kijamii na fursa za kiuchumi kwa urahisi zaidi.






No comments:
Post a Comment