Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Alban Kihulla, ametembelea Maonesho ya Wakulima (NaneNane) yanayofanyika kitaifa katika uwanja wa Nzuguni, Jijini Dodoma, leo tarehe 8 Agosti 2025.
Katika ziara hiyo, Kihulla alifika katika banda la WMA na kuwapongeza watumishi wa Wakala kwa kazi nzuri ya kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya vipimo, tangu kuanza kwa maonesho hayo. Alieleza kuridhishwa na namna Wakala unavyoshiriki kikamilifu katika kutoa elimu ya vipimo kwa wananchi.
Aidha, alisisitiza kuwa utoaji wa elimu kuhusu matumizi sahihi ya vipimo haupaswi kuishia kwenye maonesho pekee, bali uendelezwe katika ngazi zote za jamii kwa lengo la kuhakikisha haki inapatikana kwenye mnyororo mzima wa biashara na huduma.
"Ni muhimu jamii ikaelewa ni kwa namna gani Serikali kupitia WMA inawalinda kwa kuhakikisha vipimo vinavyotumika katika sekta mbalimbali ni sahihi na vinatumika kwa usahihi," aliongeza.
Mbali na kutembelea banda la WMA, Kihulla pia alifanya ziara katika mabanda mengine mbalimbali, yakiwemo ya Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, ili kujionea huduma na bidhaa zinazotolewa kwa wananchi.
Maonesho ya NaneNane hutoa fursa kwa taasisi za serikali, binafsi na wananchi kushiriki katika kubadilishana maarifa, teknolojia na huduma mbalimbali zinazolenga kuendeleza sekta ya kilimo na viwanda nchini.




No comments:
Post a Comment