Pindi Chana Ahamasisha Watanzania Kutembelea Maonesho ya Nanenane 2025

 


Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana ametoa wito kwa Watanzania kutumia ipasavyo fursa ya maonesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi (Nanenane 2025), ili kujifunza mbinu bora za uzalishaji na kuongeza thamani ya mazao kwa manufaa ya jamii na maendeleo ya taifa.



Akizungumza tarehe 4 Agosti 2025 katika viwanja vya Nanenane Nzuguni jijini Dodoma, Dkt. Chana alisema maonesho hayo yanaelimisha wananchi kuhusu uzalishaji bora wa mazao, pamoja na kukuza utalii wa vyakula.

"Naomba nitoe rai kwa Watanzania tutembelee maeneo haya ya maonesho, kuna bidhaa nzuri, kuna utafiti, kuna elimu, kuna mbegu, vivutio vya kila aina na pia unapokuja katika maonesho haya unapata elimu ya aina mbalimbali," alisema Dkt. Chana.



Aliongeza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Kilimo ili kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa mazao na kuongeza mapato kwa taifa na wananchi, sambamba na kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

"Tunapozalisha bidhaa tunaongeza thamani, tutapata na mapato, lakini tunataka watalii waje kuona utajiri wa Tanzania wa vyakula mbalimbali. Ndiyo maana leo tumekuwa na mabanda mahali hapa kuonesha bidhaa zetu za Wizara ya Maliasili na Utalii. Tunataka waje kuona utalii wa vyakula, kama ni chai yote hiyo ni aina ya utalii," alieleza.



Katika hatua nyingine, Waziri Chana alibainisha kuwa wizara yake inaendelea kutekeleza mikakati ya kupunguza migogoro baina ya binadamu na wanyama wakali kwa kutumia teknolojia rafiki na kutenga maeneo maalumu ya kuwalinda wananchi.

"Wizara itaendelea kutenga maeneo maalumu na kutumia ndege nyuki ili kuepusha mwingiliano na migogoro ya mara kwa mara kati ya wananchi na wanyama pori, hususan wale wakali na waharibifu," alisema Dkt. Chana.



Aidha, alitoa pongezi kwa Wizara ya Kilimo kwa kufanikisha maonesho hayo katika kanda mbalimbali nchini, hatua inayowapa fursa Watanzania wengi kujifunza mbinu bora za kilimo, ufugaji na uvuvi.

"Ni jambo la kupongeza kuwa sasa hivi tuna maonesho ya Nanenane katika kanda zaidi ya nane. Hii ni fursa kwa Watanzania wengi zaidi kupata elimu, kushiriki ubunifu, na kubadilishana uzoefu kwenye sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi," alisema.

Maonesho ya Nanenane huandaliwa kila mwaka kuanzia tarehe 1 hadi 8 Agosti kwa lengo la kuhamasisha maendeleo ya sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi kwa kutumia maarifa ya kitaalamu, ubunifu na teknolojia ili kuongeza uzalishaji na tija kwa taifa.

0 Comments:

Post a Comment