Dogo Janja Aibuka Kidedea Kura za Maoni Ngarenaro, Amshinda Diwani Aliyemaliza Muda Wake



Abdulazizi Abubakari Chende, anayefahamika zaidi kwa jina la kisanii Dogo Janja, ameibuka mshindi wa kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na sasa ndiye mgombea rasmi wa udiwani wa Kata ya Ngarenaro katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.

Katika kura hizo zilizofanyika leo, Jumatatu tarehe 4 Agosti 2025, msanii huyo maarufu wa muziki wa kizazi kipya aliyebadili mwelekeo na kuingia kwenye siasa, amepata kura 76 na kuwaacha mbali wapinzani wake, wakiwemo wanasiasa wakongwe waliowahi kushika nafasi ya uongozi ndani ya kata hiyo.

Kwa mujibu wa wasimamizi wa uchaguzi huo wa ndani ya CCM, Saphia Islam na Rajab Mwaliko, aliyeshika nafasi ya pili ni diwani aliyemaliza muda wake, Isaya Doita, aliyepata kura 60, huku Benjamin Mboyo aliyeshika nafasi ya tatu akipata kura 2 pekee.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Dogo Janja alieleza kuwa ushindi huo si wa kwake binafsi, bali ni ushindi wa vijana na wananchi wote wa Ngarenaro wanaotamani mabadiliko yenye tija.

"Ushindi huu ni wa kila kijana wa Ngarenaro, ni wa kila mama, baba na mzazi anayetamani kuona mabadiliko ya kweli. Tumekuwa tukisema kwa muda mrefu, sasa wakati umefika wa kuonesha kazi kwa vitendo," alisema Dogo Janja kwa bashasha.

Dogo Janja ambaye amekuwa akiitumia sanaa yake kuhamasisha na kuelimisha jamii, amejijengea jina kubwa kwa kuzungumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili wakazi wa Ngarenaro kupitia majukwaa ya muziki na siasa.

Katika kampeni zake za ndani ya chama, amekuwa akitumia kaulimbiu isemayo "Nguvu ya Kijana, Maendeleo ya Ngarenaro", ambapo aliahidi kushirikiana na wananchi kuleta maendeleo ya kweli, mshikamano na kuzingatia sauti za watu katika maamuzi ya maendeleo ya kata hiyo.

"Ngarenaro inahitaji uongozi wa kisasa, unaosikiliza wananchi na kutumia maarifa katika kutatua matatizo. Nimejifunza mengi kupitia muziki, kupitia jamii, na sasa naomba fursa ya kutenda," alisema Dogo Janja.

Kata ya Ngarenaro ni miongoni mwa kata za mijini zinazounda Jiji la Arusha, ikijulikana kwa historia ya siasa kali, ushindani mkubwa na mwamko wa kisiasa miongoni mwa vijana.

Kwa ushindi huu, Dogo Janja sasa anabeba bendera ya CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, ambapo atachuana na wagombea kutoka vyama vingine katika harakati za kuwania nafasi ya Udiwani.

Wananchi wengi waliokuwepo katika eneo la uchaguzi wameonyesha matumaini makubwa kwa Dogo Janja, wakimwelezea kama kielelezo cha kizazi kipya kinachojitokeza kuchukua nafasi katika uongozi wa kisiasa nchini.

0 Comments:

Post a Comment