Tuesday, August 12, 2025

Kihongosi Asikiliza Kero za Wananchi, Aagiza Afisa Mtendaji Kuondolewa Kituoni

 


Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi, ameendesha mkutano wa hadhara katika viwanja vya Soko Kuu, Kata ya Mjini Kati, uliowakutanisha mamia ya wakazi wa jiji la Arusha ili kusikiliza kero na changamoto zao na kuchukua hatua za papo kwa hapo, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha wananchi wanapatiwa suluhisho la matatizo yao kwa haraka.



Mkutano huo uliofanyika Agosti 12, 2025, ulihudhuriwa na wakuu wa idara, viongozi wa wilaya, na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za umma.

Akizungumza na wananchi, RC Kihongosi alisema:

“Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inalenga kusikiliza wananchi wake na kutatua matatizo kwa wakati. Ndio maana leo tumekuja na wataalamu wote ili kila kero ipate majibu hapa hapa.”

Katika hatua ya kusimamia uwajibikaji, RC Kihongosi aliamuru kuondolewa mara moja kwa Afisa Mtendaji wa Kata ya Mjini Kati, Simon Goodluck Nnko, kutokana na kushindwa kusimamia vema majukumu yake kwa wananchi.



Changamoto zilizotolewa na wananchi wengi zilihusu matatizo binafsi, hususan madai ya fedha na ugumu wa maisha, huku kero za kisekta zikiwa chache—jambo ambalo Kihongosi alisema linaonesha wazi kuwa serikali imepiga hatua katika kushughulikia masuala ya huduma za kijamii.

Baada ya kusikiliza kero hizo, Kihongosi alitoa maelekezo kwa viongozi husika kutatua matatizo mengine mara moja, huku mengine yakipangiwa muda wa utekelezaji. Mfano, kuhusu kero za ubovu wa miundombinu, alisema atashughulikia suala hilo binafsi.



Akihimiza mshikamano, RC alisema:

“Maendeleo ya mkoa wetu hayataletwa na mtu mmoja, bali kwa ushirikiano wa kila mmoja wenu. Endeleeni kushirikiana na serikali kwa kutoa taarifa za matatizo mapema, kushiriki katika shughuli za maendeleo, kulinda amani, na kuepuka vurugu au maandamano yasiyo na tija.”

 

Awali kabla ya mkutano huo, RC Kihongosi alitembelea miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa jengo jipya la utawala la Jiji la Arusha lenye ghorofa 7, Kituo cha Damu Salama, na jengo la wagonjwa wa saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru.

No comments:

Post a Comment