ARUSHA – Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi, amepongeza hatua ya ujenzi wa jengo jipya la utawala la Jiji la Arusha lenye ghorofa saba, huku akisisitiza kuwa mradi huo unapaswa kukamilika ifikapo Mei 2026 bila kuongezewa muda mwingine wa utekelezaji.
Akizungumza Agosti 12, 2025 wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo pamoja na miradi mingine ya maendeleo jijini Arusha, Kihongosi alisema jengo hilo lina ubora wa hali ya juu na linagharimu shilingi bilioni 9.852, ambapo hadi sasa halmashauri imeshatoa shilingi bilioni 2.84 kupitia mapato ya ndani.
“Mradi una sifa zote za kuwa bora, kwa macho unaweza kuona quality ya ujenzi. Gharama za mradi zinaendana na ubora wake. Nayasema haya kwa sababu nimekagua miradi ya mwenge nchi nzima mwaka 2019. Unaona fedha imetumika vizuri sana, hongereni sana,” alisema Kihongosi.
Alimtaka mkandarasi wa mradi huo, kampuni ya M/S Tribe Construction Ltd, kuhakikisha anatekeleza wajibu wake kwa ukamilifu na bila uzembe, akisisitiza kuwa muda wa nyongeza wa miezi mitatu walioomba baada ya tarehe ya awali ya kukamilika mwezi Septemba, uwe wa mwisho.
“Mkandarasi amenieleza kuwa structure inakamilika mwezi wa tisa lakini wameomba extension ya miezi mitatu. Nimemwambia Mkurugenzi hiyo iwe ya mwisho. Muanze kumkata anayozembea kuyatekeleza katika mradi. Jengo hili inabidi likamilike mwezi wa tano mwakani lianze kutumika,” aliongeza.
Kihongosi pia alitumia nafasi hiyo kumpongeza Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, John Kayombo, kwa usimamizi madhubuti wa mradi na kueleza matumaini yake kuwa jengo hilo litawezesha watumishi wote wa jiji kupata mazingira bora ya kufanyia kazi.
“Mkurugenzi John Kayombo nakupongeza sana. Najua kuna baadhi ya watumishi wanatumia majengo ya kata. Ujenzi huu ukikamilika watumishi wote wa jiji watapata nafasi. Nimesikia kwenye basement kuna sehemu ya kuegesha magari zaidi ya 100, hongereni sana,” alisema.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mkandarasi, jengo hilo litakuwa na lifti na mgahawa, jambo ambalo linatarajiwa kuongeza ufanisi na ustawi wa watumishi wa umma pamoja na wananchi wanaofika kupata huduma.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alitoa wito kwa viongozi wa umma kusimamia na kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuzingatia maadili ya kazi ili kuacha kumbukumbu nzuri wanapomaliza muda wao wa utumishi.
“Kuna baadhi ya watu kazi yao kubwa ni maneno maneno. Ukija mkuu wa mkoa mpya, ameshakuja na mafaili ya watu. Nawaomba msiniletee hayo. Nitawajua kwa kufanya nao kazi. Tukutane mezani na tuwe wawazi,” alisisitiza.
Pia alionya tabia ya baadhi ya watumishi kutumia mahusiano yao na viongozi wa juu kuvuruga taratibu za utumishi wa umma.
“Unakuta kuna mkuu wa idara anafahamiana na waziri fulani, anamwambia Mkurugenzi nimepigiwa simu nifanye hivi. Hapana. Mwambie mkuu, ‘usinichonganishe na mkuu wangu wa kazi, mpigie mwenyewe.’ Tuheshimu taratibu,” alionya.
Katika nasaha zake kwa watumishi wa umma, Kihongosi aliwataka kuishi maisha ya uwazi na furaha, huku akiwahimiza kutumia vizuri fursa ya kufanya kazi mkoani Arusha.
“Mtumishi wa umma, fanya kazi kwa uaminifu, kwa spidi kubwa. Nenda kalale Gran Melia siyo dhambi, nenda Mount Meru au Kibo Palace siyo dhambi. Unakaa miaka mitano Arusha hujawahi kwenda Ngorongoro kuangalia wanyama? Hiyo siyo sawa,” alisema huku akisisitiza kuwa maisha ya mtumishi wa umma yanapaswa kuwa ya mfano na heshima.
Kuhusu uchaguzi ujao, Kihongosi aliwahimiza watumishi na wananchi kushiriki kwa ufanisi na kuwachagua viongozi wazalendo, wachapakazi, wenye hofu ya Mungu na wanaoipenda nchi.
“Tunahitaji kumuunga mkono Mheshimiwa Rais. Mtumishi wa umma usiwe sehemu ya wanaoisema serikali, kwa sababu na wewe ni sehemu ya serikali. Tuieleze vizuri kwa kutekeleza wajibu wetu,” alisema.
Kiongozi huyo alimaliza kwa kupongeza ushirikiano wa viongozi wa Jiji la Arusha na kuwataka waendelee kushirikiana kwa ajili ya maendeleo ya mkoa na wananchi wake.
“Kayombo, nakupongeza kwa kazi nzuri sana kuhakikisha Arusha inabadilika. Watumishi, naomba mumpe ushirikiano. Chini ya Mkuu wa Wilaya Mkude, Mkurugenzi Kayombo na watumishi, naamini lengo hili litafikiwa,” alihitimisha.
Jengo la utawala la Jiji la Arusha linatarajiwa kuwa miongoni mwa majengo ya kisasa ya halmashauri nchini na litasaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi pamoja na mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma.





No comments:
Post a Comment