Dar es Salaam – Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Paramagamba Kabudi, ametaja majukumu makuu matano ambayo sekta ya habari inapaswa kuyatekeleza kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Akizungumza katika Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Habari na Utangazaji Kanda ya Mashariki, Profesa Kabudi alisema vyombo vya habari vina wajibu mkubwa katika kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa haki, amani na uwazi.
“Jukumu la kwanza ni kuwajulisha wananchi kuhusu haki na wajibu wao. La pili ni kutoa elimu juu ya sera za wagombea. La tatu ni kuibua na kufuatilia ukiukwaji wa sheria za uchaguzi. La nne ni kuhamasisha ushiriki wa makundi maalum hususan vijana na wanawake, na la tano ni kupambana na taarifa potofu na kuepuka kuzisambaza,” alisema Profesa Kabudi.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa majukumu hayo unapaswa kuzingatia taaluma, weledi na maadili ya uandishi wa habari, akisisitiza kuwa waandishi wanapaswa kuwa sehemu ya kulinda amani na mshikamano wa taifa katika kipindi chote cha uchaguzi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, Wakili Patrick Kipangula, alitoa angalizo kwa wanahabari kuzingatia matakwa ya kisheria kabla ya kushiriki kuripoti habari za uchaguzi.
“Ni kosa la jinai kwa mwandishi kufanya kazi bila ithibati. Kifungu cha 19 cha Sheria ya Huduma za Habari kinaeleza kuwa mtu yoyote anayetaka kufanya kazi za uandishi wa habari lazima awe amepewa ithibati na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari. Hivyo waandishi wote wanaotarajia kuripoti uchaguzi wahakikishe wana ithibati,” alisema Kipangula.
Mkutano huo uliwaleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya habari na utangazaji kutoka Kanda ya Mashariki, ambapo washiriki walijadili nafasi ya vyombo vya habari katika kusimamia mchakato wa uchaguzi kwa uwazi, pamoja na kuimarisha uelewa wa wananchi katika kushiriki kidemokrasia.




No comments:
Post a Comment