Thursday, August 21, 2025

DARAJA LA MOHORO KUWA MSAADA MKUBWA KWA WANANCHI – BODI TARURA YAIPONGEZA SERIKALI

 


Rufiji, Pwani
Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeipongeza Serikali kwa kuwezesha ujenzi wa daraja la Mohoro wilayani Rufiji, daraja ambalo linatajwa kuwa mkombozi kwa mawasiliano na maendeleo ya kiuchumi kwa wakazi wa eneo hilo.


Akizungumza katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa mita 100 pamoja na barabara za lami kilomita 4 zinazojengwa katika mji wa Ikwiriri, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhandisi Florian Kabaka alisema:

“Niipongeze serikali kwa uwezeshaji huu kwa TARURA, kwakweli uwepo wake hata wananchi wanaishukuru kwa kufungua miundombinu kila mahali, nitoe heko kwa serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa TARURA pia nitoe heko kwa menejimenti ya TARURA kwa usimamizi.”


 

Aidha, Mhandisi Kabaka aliwasihi wananchi wa Mohoro kuhakikisha wanatunza daraja hilo na vifaa vyote vya miundombinu vinavyolizunguka ili liweze kudumu na kuhudumia vizazi vijavyo.

“Daraja hili linaenda kuwaondolea shida iliyodumu kwa miaka mingi lakini kuwafungulia fursa ya kujenga uchumi wao na Taifa kwa ujumla.”


 

Aliongeza kuwa TARURA itaendelea kuondoa vikwazo vya usafiri na usafirishaji nchini kwa kupanua mtandao wa barabara, hatua itakayowawezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kuinua uchumi.





Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Mkoa wa Pwani, Mhandisi Leopold Runji alisema ujenzi wa daraja hilo utakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Mohoro na maeneo jirani.

“Mradi huu unaenda kuwasaidia wananchi kwani shughuli nyingi za ukanda huu ni uchumi wa blue pamoja na kilimo cha mazao mchanganyiko, hivyo kukamilika kwa daraja hili kutaondoa vikwazo vya muda mrefu.”

Naye Mhandisi Mkazi wa mradi huo, Emmanuel Mahimbo alieleza kuwa kazi ya ujenzi inaendelea vizuri na hadi sasa imefikia asilimia 48.



“Tayari tumeshakamilisha ujenzi wa boksi kalavati mbili, nguzo nne na sasa tunaongeza nguzo nyingine.”

Alifafanua kuwa mkandarasi ameanza kuingiza mashine zaidi na kuongeza wafanyakazi ili kuhakikisha kazi inakwenda kwa kasi na kufikia lengo la kukamilisha sehemu ya daraja ifikapo Januari 2026.



“Mpango kazi wetu hadi kufikia mwezi Januari 2026 ni kuhakikisha sehemu ya daraja imekamilika ili tuweze kubaki na kazi ya kumalizia barabara.”

Wananchi wa Mohoro wameshauriwa kutunza daraja hilo mara baada ya kukamilika kwa kuwa litakuwa kiunganishi muhimu cha uchumi, huduma za kijamii na maendeleo kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment