Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la kisasa la ghorofa nane la Kituo cha Jiomolojia Tanzania (TGC), linaloendelea kujengwa jijini Arusha.
Jengo hilo litagharimu zaidi ya Shilingi bilioni 33 hadi kukamilika kwake, na linatajwa kuwa miongoni mwa miradi ya kimkakati inayolenga kuimarisha Sekta ya Madini nchini.
Katika ziara hiyo, Mavunde alieleza kuwa lengo la ujenzi wa jengo hilo ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na uongezaji thamani wa madini ya vito na madini mengine Afrika Mashariki, sambamba na kuimarisha miundombinu ya kitaaluma na kiteknolojia katika sekta hiyo.
"Mradi huu ni wa kimkakati kwa mustakabali wa Sekta ya Madini nchini ambao utawaleta pamoja wafanyabiashara wa madini (One Stop Centre). Tunahitaji kuona ujenzi ukikamilika haraka ili kituo hiki kianze kufanya kazi kama ilivyokusudiwa," alisema Mavunde.
Jengo la kisasa lenye miundombinu ya elimu na biashara ya madini
Mradi wa jengo la TGC unatekelezwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Madini kwa kushirikiana na taasisi ya TGC. Jengo hilo linatarajiwa kuwa na:
-
Madarasa ya kufundishia wanafunzi wa masuala ya jiolojia na jiomolojia
-
Karakana za mafunzo kwa vitendo
-
Maabara ya kisasa ya uchambuzi wa madini
-
Mabweni ya wanafunzi
-
Ofisi za uongozi wa chuo
-
Nafasi za biashara ya madini kwa mfumo wa One Stop Centre
Kwa mujibu wa Mhandisi Julian Mosha kutoka kampuni ya Skywards Lumocons Joint Venture, ujenzi unaendelea kwa hatua nzuri. Hata hivyo, Waziri Mavunde alitoa maelekezo ya kuongeza kasi na ufanisi wa kazi.
"Natoa wito kwa mkandarasi kuongeza nguvu kazi, vifaa na ufanisi ili kuendana na muda wa mkataba," alisema Mavunde.
Msimamizi wa mradi kutoka TGC, Jumanne Nshimba, alieleza kuwa mradi huo ukikamilika utaongeza uwezo wa kitaifa wa kutoa mafunzo ya kitaalamu na kuchambua madini kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Wadau wa madini wapongeza jitihada za Serikali
Uongozi wa Chama cha Wafanyabiashara Wadogo wa Madini ya Vito (CHAMATA) na Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Arusha (AREMA) walishukuru kwa ujenzi huo na ujio wa Waziri wenye lengo la kusikiliza changamoto na mapendekezo yao kuhusu biashara ya madini.
"Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza kwenye ujenzi huu wa kihistoria. Jengo hili litazalisha wataalamu wazawa na kurahisisha biashara ya madini kwa kuwa litawakutanisha wadau wote kwa wakati mmoja," alisema Alfred Mwaswenya, Mwenyekiti wa AREMA.
"Hili jengo litasaidia sana wafanyabiashara wa madini kupata huduma zote kwa pamoja, kutoka ujuzi hadi soko. Ni hatua kubwa ya maendeleo kwa sekta yetu," alisema Jeremia Kituyo, Mwenyekiti wa CHAMATA.
Uwekezaji wa Serikali katika miundombinu ya madini
Waziri Mavunde alipokea taarifa za utekelezaji wa shughuli za madini mkoani humo akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi ambaye alitumia fursa hiyo kumpongeza Waziri na Serikali kwa ufuatiliaji wa karibu wa maendeleo ya sekta ya madini.
"Serikali kupitia Wizara ya Madini imeonyesha dhamira ya kweli kwa kuwekeza kwenye miundombinu ya kisasa kama hili jengo la TGC. Hili ni jambo la kupongeza na litaongeza thamani ya madini na kuinua uchumi wa wananchi wa Arusha," alisema Kihongosi.
Aidha, Waziri Mavunde alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza mkakati wa kuimarisha matumizi ya kisayansi ya rasilimali za madini nchini kwa kukuza elimu, ujuzi na teknolojia.
"Tuna dhamira ya kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha biashara ya madini Afrika, kwa kutumia ujuzi na teknolojia ya kisasa ili kuongeza thamani ya madini yetu kabla ya kuuzwa," aliongeza Mavunde.
Mradi huu wa jengo la TGC unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya sekta ya madini, kuongeza ajira kwa vijana wa Kitanzania, na kuongeza mapato ya serikali kupitia mauzo ya madini yaliyoongezwa thamani.








No comments:
Post a Comment