Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenani Laban Kihongosi, amepiga marufuku matumizi ya vifaa vinavyotoa milio ya fataki kwenye pikipiki maarufu kama bodaboda pamoja na biashara ya tatu mzuka, akisisitiza kuwa vitendo hivyo vinahatarisha usalama na ustawi wa wakazi wa mkoa huo.
Akizungumza Julai 22, 2025, katika mkutano wa wazi na madereva wa bodaboda, bajaji na magari madogo uliofanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Kihongosi alitoa siku tatu kwa madereva hao kuondoa vifaa hivyo kwenye vyombo vyao vya usafiri, akitaja kuwa kelele hizo ni kero kwa jamii.
“Nimeletwa kero hii na wazee na viongozi wetu wa dini. Unapopiga fataki hiyo, kumbuka kelele hizo zinaleta usumbufu mkubwa kwa watu wanaosikia – kuna wagonjwa, kuna wazee, na wengine wenye changamoto. Fanyeni utaratibu wa kuondoa kifaa hicho. Natoa siku 3 kama mlivyokubaliana hapa.”
Aliweka bayana kuwa kelele hizo za ghafla, zinazoambatana na sauti ya milipuko, zimekuwa zikitia hofu watalii, kuharibu sura ya jiji na kuvuruga utulivu wa wakazi wa maeneo ya mijini na pembezoni.
“Milio hiyo si salama, inatisha wananchi na kuharibu taswira ya mji wetu wa utalii. Tutafuatilia na kuchukua hatua kwa yeyote atakayekiuka agizo hili.”
Katika hatua nyingine, Kihongosi alisisitiza kuwa biashara ya tatu mzuka haina nafasi ndani ya Mkoa wa Arusha, akiwataka vijana kuacha mara moja kujihusisha na shughuli hiyo haramu isiyokuwa na tija.
“Wanaofanya biashara haramu ya tatu mzuka waache mara moja. Heshimuni kazi yenu ili wengine waiheshimu. Serikali inaithamini kazi yenu ya usafirishaji, lakini wanaokwenda kinyume hawatakuwa salama.”
Akiwahutubia mamia ya madereva waliohudhuria mkutano huo, Kihongosi aliwataka waheshimu kazi yao kwa kuitambua kama ajira halali yenye nafasi kubwa ya kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Tumieni kazi yenu kuwaletea maendeleo. Tumieni fedha vizuri kwa kuwa na malengo ya kimaendeleo. Nyinyi ni vijana, twendeni tukafanye maendeleo.”
Aidha, aliwasihi kuwa chanzo cha taarifa kwa vyombo vya usalama kwa sababu ya mwingiliano wao na watu wa kada tofauti kila siku.
“Kazi hii mnayoifanya inatakiwa kuwapa kipato nyie na heshima ya Taifa hili. Lindaneni ninyi kwa ninyi. Wapo wageni wa ndani na nje ya nchi wanaotumia usafiri huu – fanyeni kazi hii kwa nidhamu na weledi mkubwa.”
Alieleza kuwa usalama wa mkoa huo ni jambo la msingi katika kukuza uchumi na hasa sekta ya utalii, hivyo ni muhimu kwa kila dereva kuwa mlinzi wa amani ya jiji.
“Mnapakia watu wengi. Mnapaswa kuwa na masikio ya taifa. Toeni taarifa mapema kwa vyombo vya usalama badala ya kushiriki au kuficha uhalifu.”
Kihongosi alisisitiza pia umuhimu wa kuvaa kofia ngumu (helmet) wakati wote wa kuendesha pikipiki kwa ajili ya usalama wa madereva hao, na kuwataka kutoshiriki michezo ya kuwakimbia askari barabarani.
“Miili yenu ni mali ya Taifa hili, lazima ilindwe. Kazi yenu ni ajira kama kazi nyingine, msikubali kugawanywa na mtu yeyote wakiwemo wanasiasa.”
Katika hotuba yake, RC huyo alitoa onyo kali kwa vibaka na wezi wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu jijini humo.
“Nawaambia wazi, kazi hiyo si salama. Mkoa huu hautakuwa sehemu ya watu wanaoamua kufanya uhalifu na kuharibu amani. Hatuwezi kukuza utalii kama mgeni anakuja na kuibiwa.”
Aliagiza Kamanda wa Polisi Wilaya (OCD) kutowavumilia watu wanaovunja sheria kwa makusudi, huku akisisitiza kuwa Arusha lazima ibaki kuwa sehemu salama kwa raia na wageni.
Kwa upande wao, madereva walitumia nafasi hiyo kueleza changamoto wanazokutana nazo, ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwa baadhi ya vituo vya kupakia abiria, kuzuiwa kutumia njia kadhaa, na kukosa maeneo rasmi ya kupaki vyombo vyao.
Walimwomba Mkuu wa Mkoa kuingilia kati kwa ajili ya kutambua rasmi maeneo ya kupaki pamoja na kurudisha njia walizozuiwa.
Akijibu hoja hizo, Kihongosi aliahidi kulifanyia kazi suala hilo, na kuahidi kukutana nao tena kabla ya mwezi wa tisa ili kutoa mrejesho wa maamuzi ya Serikali.
“Tutakutana tena kabla ya mwezi wa tisa. Lengo letu ni kutatua changamoto zenu kwa haki, lakini pia kuhakikisha sheria na taratibu zote zinafuatwa.”
Mkutano huo umeonyesha dhamira ya serikali ya kushirikiana moja kwa moja na sekta isiyo rasmi ili kuhakikisha Arusha inaendelea kuwa kitovu cha amani, utalii na ajira zenye heshima kwa vijana.










No comments:
Post a Comment