Saturday, July 19, 2025

TANZANIA YAZIDI KUNG'AA: MRADI WA URANI KUCHOCHEA UZALISHAJI WA UMEME NA MAENDELEO RUVUMA



Serikali imepiga hatua kubwa katika sekta ya madini kwa kuanza utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa uchimbaji na uchenjuaji wa madini ya urani wilayani Namtumbo, mkoani Ruvuma, mradi unaotarajiwa kuongeza uzalishaji wa umeme nchini na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10 bora duniani kwa uzalishaji wa madini hayo muhimu.



Akizungumza tarehe 18 Julai 2025 akiwa katika ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde alieleza kuwa ujenzi wa kiwanda cha majaribio cha uchenjuaji wa urani umekamilika, hatua inayowezesha kuanza kwa mradi huo mkubwa wa kiuchumi.

"Moja kati ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya madini ni suala la uongezaji thamani madini ndani ya nchi yetu, na Rais ametupa maelekezo mahsusi Wizara kusimamia hili," alisema Mavunde.



Mradi huo unaotekelezwa na Kampuni ya Mantra Tanzania Limited, unakadiriwa kugharimu zaidi ya shilingi trilioni 3.06 hadi kukamilika kwake. Mashapo ya urani katika eneo hilo yanakadiriwa kufikia tani milioni 139, hali inayokadiri maisha ya mgodi huo kufikia miaka 22, na hivyo kuimarisha nafasi ya Tanzania katika soko la kimataifa la madini ya urani.

"Kuanza kwa mradi huu ambao unahusisha pia ujenzi wa kiwanda cha kuongeza thamani madini ya urani unadhihirisha utekelezaji wa azma ya Serikali kwa vitendo. Katika hili, sisi Wizara ya Madini tutaendelea kusimamia kikamilifu ili kunufaisha nchi yetu," aliongeza Mavunde.




Waziri huyo pia alieleza kuwa mbali na mapato yatakayopatikana, mradi huo unatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 4,000 za moja kwa moja na zaidi ya 100,000 zisizo za moja kwa moja, huku kampuni ya Mantra ikiendelea na majadiliano na Serikali kwa lengo la kujenga mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia urani itakayochimbwa.



Aidha, Mavunde alisema: "Mradi huu unakwenda kubadilisha taswira ya Namtumbo kwani unakwenda kugusa maisha ya wananchi wengi wanaozunguka mradi."



Kwa upande wake, Meneja wa Uendelezaji Mradi kutoka Mantra, Majani Moremi, alieleza kuridhishwa kwao na ushirikiano wanaopata kutoka Serikali.



"Serikali imeendelea kutoa ushirikiano kwa kampuni yetu, hali iliyowezesha kufanikisha kuanza kwa mradi huu. Tunaahidi kuwa mradi huu utaleta tija na mafanikio tarajiwa kwa nchi," alisema Moremi.

Nao viongozi wa mkoa wameelezea kufurahishwa kwao na utekelezaji wa mradi huo mkubwa. Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas alisema:
"Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji nchini yaliyopelekea mradi huu kutekelezwa mkoani Ruvuma. Tutaendelea kutoa ushirikiano kwa Kampuni ya Mantra muda wote ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huu kwa manufaa ya nchi na wananchi wa Namtumbo."


Mradi huu unaashiria mwanzo wa zama mpya za uchumi wa madini nchini, na unatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuzalisha nishati ya kutosha kwa maendeleo ya viwanda, huduma na maisha ya wananchi kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment