Morogoro, Julai 24, 2025 – Serikali kupitia Wizara ya Madini imemkabidhi Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) leseni ya utafiti na uchimbaji mkubwa wa madini adimu ya Rare Earth Elements (REE) katika eneo la Vilima vya Wigu, Wilaya ya Morogoro. Hii ni hatua muhimu inayolenga kuendeleza sekta ya madini kwa manufaa ya taifa na wananchi wake.
Makabidhiano hayo yamefanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Sesenga, Kijiji cha Sesenga, Kata ya Mgazi, na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali na sekta ya madini.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema leseni hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kuongeza uwekezaji wa STAMICO katika madini ya kimkakati.
“Madini ya Rare Earth Elements ni rasilimali muhimu sana inayotumika katika vifaa vya teknolojia ya kisasa kama simu za mkononi, kompyuta, betri za magari ya umeme, vifaa vya matibabu na hata vifaa vya kivita,” amesema Waziri Mavunde. “Ni fursa kubwa kwa wananchi wa kijiji cha Sesenga, Wilaya ya Morogoro na Taifa kwa ujumla kupata manufaa kutoka kwenye madini haya.”
Waziri Mavunde pia amebainisha kuwa mradi huu utafungua fursa nyingi za ajira kwa wakazi wa maeneo jirani na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Amesisitiza pia umuhimu wa kuzingatia sera za local content na uwajibikaji wa kijamii (CSR) kwa kuhakikisha wananchi wa maeneo yanayozunguka migodi wanapata kipaumbele katika ajira na biashara zinazohusiana na mradi.
Aidha, amebainisha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro itapata mapato zaidi kupitia tozo za huduma zitakazotozwa kwenye shughuli za madini, na hivyo kuimarisha huduma za kijamii katika maeneo hayo.
Katika hotuba yake, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, amempongeza Waziri Mavunde kwa usimamizi wake mzuri wa sekta ya madini na kuahidi kushirikiana kwa karibu katika kufanikisha maendeleo ya mradi huu kwa manufaa ya taifa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuunda mazingira rafiki na salama ya uwekezaji katika sekta ya madini nchini.
Amesema, “Kwa sasa wachimbaji wa madini wananufaika moja kwa moja na rasilimali za nchi hii, jambo ambalo ni chachu ya maendeleo endelevu.”
Uamuzi wa Serikali kukabidhi leseni hiyo kwa STAMICO umetokana na ushindi wa Tanzania katika kesi ya utata wa leseni iliyokuwa mikononi mwa kampuni ya Wigu Hill Mining Company Limited, kufuatia mchakato wa usuluhishi wa migogoro ya uwekezaji (ICSID).
Hatua hii ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba rasilimali za madini zinatumiwa kwa manufaa ya taifa, zikiendelezwa ipasavyo na wananchi wanapata fursa za kiuchumi kutokana na uwekezaji huo.




No comments:
Post a Comment