Thursday, July 24, 2025

Majaliwa Avutia Uwekezaji Mpya Kutoka Belarus: “Tanzania Iko Tayari”

  


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili nchini Belarus kwa mafanikio makubwa, akitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wa sekta mbalimbali kuja kuwekeza Tanzania, huku akisisitiza kuwa serikali iko tayari kushirikiana kwa karibu na wawekezaji hao kwa maendeleo ya taifa.



Katika ziara hiyo, Majaliwa alikutana na wakuu wa taasisi na kampuni kubwa nchini humo, ambapo alieleza maeneo ya kimkakati ambayo Tanzania inakaribisha uwekezaji wa moja kwa moja. Maeneo hayo ni pamoja na elimu ya juu, afya, kilimo, teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), maendeleo ya viwanda, madini na utalii.


“Tanzania imeboresha kwa kiasi kikubwa mazingira ya uwekezaji, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Serikali yetu iko tayari kutoa ushirikiano na msaada wowote wa msingi kwa wawekezaji watakaokuja nchini,” alisema Majaliwa.

Akizungumza na viongozi wa viwanda vya matrekta na mitambo ya kilimo, Majaliwa aliwataka kufungua matawi yao nchini Tanzania na kuanzisha vituo vya kutoa huduma za matrekta kwa wakulima ili kusaidia mapinduzi ya kilimo.

“Nawasihi kuanzisha mechanization centres nchini ili ziwasaidie wakulima wetu kupata huduma kwa karibu. Hili ni eneo lenye fursa kubwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa letu,” alisisitiza.



Katika siku ya mwisho ya ziara yake, Majaliwa alitembelea viwanda mbalimbali vya teknolojia ya kisasa, ikiwemo vya kutengeneza mitambo ya uchimbaji wa madini, magari ya migodini, vifaa vya zimamoto na uokoaji. Alisisitiza umuhimu wa kushirikiana na viwanda hivyo kuondoa changamoto ya uhaba wa vifaa hivyo nchini.

“Tunayo haja ya kuimarisha usalama na huduma za uokoaji nchini. Ushirikiano na viwanda hivi ni hatua muhimu katika kufanikisha hilo,” alisema.



Majaliwa pia alitembelea taasisi za uzalishaji wa dawa na vifaa tiba, viwanda vya vifaa vya kielektroniki, chuo kikuu cha kilimo cha Belarus (BSATU), na alikutana na jumuiya ya wafanyabiashara wanaofanya kazi na bara la Afrika (AFTRADE).



Katika tukio jingine muhimu, Majaliwa na mwenyeji wake, Alexander Turchin, walishuhudia utiaji saini wa makubaliano matatu ya mashauriano ya kisiasa na ushirikiano katika sekta za elimu na kilimo kati ya Tanzania na Belarus. Pia walishuhudia utiaji saini wa mkataba kati ya Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) na chama cha wafanyabiashara wa Belarus, unaolenga kukuza ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili.

Wakati wa ziara hiyo, Waziri Mkuu aliambatana na viongozi na watendaji mbalimbali wa serikali akiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – SMZ, Shariff Ali Sharriff, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Khatibu Kazungu, Naibu Katibu Mkuu wa Kilimo, Dkt. Stephen Nindi pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Urusi na Belarus, Fredrick Kibuta.

Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu aliweka shada la maua kwenye mnara wa kumbukumbu ya mashujaa wa taifa la Belarus kama ishara ya heshima na mshikamano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Belarus.

Ziara hii imefungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Belarus na inatarajiwa kuzaa matunda ya uwekezaji mkubwa katika sekta muhimu za maendeleo nchini.


No comments:

Post a Comment