Katika uchaguzi uliovuta hisia kali na kushuhudiwa na maelfu ya wanachama wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), wagombea wapya Chiku Athuman Issa na Martha Gido Kivunge wameibuka kidedea waking'oa vigogo waliokuwa wakitetea nafasi zao kwa zaidi ya miaka kumi, katika uchaguzi wa nafasi ya ubunge wa viti maalum Mkoa wa Arusha.
Uchaguzi huo uliofanyika Julai 30, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa AICC, Arusha, uliandaliwa na kusimamiwa kwa ukamilifu na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Kenani Kihongosi.
Akisoma matokeo baada ya wajumbe wapatao 1261 kupiga kura, Kihongosi alibainisha kuwa jumla ya kura 1252 zilipigwa, ambapo kura halali zilikuwa 1245 huku kura 7 zikiharibika.
WAPYA WAPETA, VIGOGO WAZIMIA
Katika matokeo hayo, Martha Gido Kivunge aliongoza kwa kura 1004, akifuatiwa na Chiku Athuman Issa aliyepata kura 775.
Ushindi huo wa kishindo uliwafanya wagombea hao wawili kuwa gumzo la uchaguzi huo na kuamsha shangwe za wajumbe waliokuwa na kiu ya mabadiliko ndani ya UWT Mkoa wa Arusha.
“Tumepata viongozi wapya. Tunatarajia kuona mtazamo mpya, uongozi mpya na mwanzo mpya wa UWT Arusha,” alisema mmoja wa wajumbe kutoka Arusha Mjini aliyeomba kutotajwa jina.
Katika orodha ya wagombea waliopigwa chini ni pamoja na Catheline Valentine Magige aliyepata kura 213 na Zaytun Seif Swai aliyepata kura 141. Magige, ambaye amewahi kuhudumu bungeni kwa zaidi ya miaka 18, anaelezwa kukumbwa na "wimbi la mabadiliko" ambalo wajumbe wengi waliamua kulikumbatia.
MCHAKATO WA UCHAGUZI NA MCHUJO WA CHAMA
Wagombea hao walikuwa miongoni mwa wanachama nane waliopitishwa na Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa na kutangazwa rasmi na Katibu wa Itikadi na Uenezi CPA Amos Makalla, Julai 29, 2025. Majina mengine ni pamoja na Dkt. Asanterabi Ngoyai Lowassa (kura 196), Navoi Mollel (95), Martha Martin Amo (50), na Lilian Joseph Badi (9).
Kwa mujibu wa taratibu za CCM, baada ya uchaguzi wa wajumbe, majina yanapitia mchujo mwingine wa ndani ambao hufanywa na vikao vya juu vya chama ili kuzingatia uwiano wa kura pamoja na usawa wa kanda na jinsia kabla ya kupendekezwa kwa nafasi za viti maalum bungeni.
CHIKU ISSA NA MARTHA GIDO – WASIFU WAO WAONGOZA MABADILIKO
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema ushindi wa Martha na Chiku umechangiwa zaidi na rekodi zao safi za utendaji na maono mapya waliyoahidi kwa UWT Arusha.
Chiku Athuman Issa amejikita katika masuala ya uchumi na usimamizi wa fedha.
Amewahi kuwa Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa Benki ya CRDB na kwa sasa ni Mjumbe wa Kamati ya Uchumi, Mpango na Fedha wa UWT Taifa, pamoja na kuwa mjumbe wa Mkutano Mkuu wa UWT Taifa na mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Wilaya ya Arusha Jiji.
Kwa upande wake, Martha Gido ni mtaalamu wa masuala ya jinsia na maendeleo ya jamii, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika harakati za kuwawezesha wanawake kiuchumi na kijamii kupitia taasisi mbalimbali za kijamii mkoani Arusha.
“Mwanamke wa leo anahitaji mtu anayemwakilisha sio kwa sura bali kwa sera. Tumechagua sera,” alisema mjumbe mmoja kutoka Longido.
ANGUKO LA WALIOTETEA NAFASI
Habari kutoka kwa baadhi ya wajumbe zinaeleza kuwa kuanguka kwa Catheline Magige na Zaytun Swai kulichangiwa na siasa za makundi na mvutano wa ndani wa muda mrefu ambao umekuwa ukilalamikiwa na wanachama kwa muda mrefu.
“Wanawake wa Arusha wamechoshwa na siasa za uswahiba. Wanahitaji uongozi wa kweli. Hawa wamepewa nafasi, hawakutenda, sasa ni wakati wa sura mpya,” alieleza mjumbe kutoka Arumeru.
Licha ya uzoefu mkubwa aliokuwa nao, Catheline Magige anaelezwa kuwa alishindwa kuendana na mabadiliko ya kisiasa ndani ya chama, huku baadhi wakitaja kuwa mgawanyiko wa ndani wa kikundi chake ulikuwa kikwazo kikubwa katika safari yake ya kutetea kiti.
HATUA INAYOFUATA
Baada ya uchaguzi huu wa mkoa, mchakato wa chama utaendelea kwa vikao vya juu kuamua nani ataingia bungeni kupitia viti maalum kwa kuzingatia uwiano wa kura, jinsia na kanda, huku jina la Martha Kivunge likitajwa kuwa na nafasi kubwa kuendelea mbele.
Uchaguzi huu ni ishara kuwa CCM inaendelea kujiimarisha kupitia mchakato wa ndani unaolenga kutafuta viongozi wenye uwezo, weledi na maono mapya.
“Jamvi kuchanika si mwisho wa maongezi. Ila ni fundisho kwamba siasa sio urithi wa mtu mmoja, kila mmoja ana nafasi yake,” alisema mchambuzi mmoja wa siasa za chama hicho.
Kwa sasa, macho na masikio yote yako kwenye vikao vya juu vya CCM ambavyo vitatoa uamuzi wa mwisho juu ya nani atapeperusha bendera ya wanawake wa Arusha kupitia viti maalum bungeni.








No comments:
Post a Comment