Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju, amepongeza juhudi za Mfuko wa Abbot Fund kwa kushirikiana na Serikali katika kuimarisha maisha ya watoto wenye mahitaji maalum nchini.
Akizungumza Julai 30, 2025, jijini Dodoma baada ya ujumbe kutoka Abbot Fund kutembelea Makao ya Taifa ya Watoto yaliyopo Kikombo, Wakili Mpanju alisema, “Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, inatoa pongezi na shukrani kwa uongozi wa Mfuko wa Abbot Fund kwa kuendelea kushirikiana nasi ili kuwezesha kustawisha maisha ya watoto wanaolelewa katika Makao ya Taifa na jamii kwa ujumla.”
Katika ziara hiyo, Mfuko wa Abbot Fund ulikabidhi vifaa mbalimbali vya kujifunzia kwa watoto walioko katika makao hayo, vikiwemo kompyuta, madaftari na mavazi.
Wakili Mpanju alipokea vifaa hivyo kwa niaba ya Serikali na kueleza kuwa msaada huo utachangia kuboresha elimu na ustawi wa watoto hao.
Akiwaongoza wageni hao, Wakili Mpanju pia alitembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Makao hayo ikiwemo mradi wa kilimo, ufugaji wa samaki na karakana ya ushonaji, ambapo watoto hupata mafunzo ya stadi za maisha. “Kupitia miradi hii, watoto wanajifunza ujuzi muhimu wa kujitegemea baada ya kuhitimu maisha ya malezi katika makao haya,” alisema.
Kwa upande wake, Makamu Mkurugenzi wa Mfuko wa Abbot Fund, Julia Gin, aliahidi kuendeleza ushirikiano huo na Serikali. “Tutaendelea
kushirikiana na Serikali kuhakikisha watoto wanaolelewa katika makao wanapata huduma stahiki na stadi za maisha zitakazowasaidia katika maisha yao ya baadaye,” alisema.





No comments:
Post a Comment