MBATIA AIBUKA KIDEDEA: MAHAKAMA YAMREJESHA MADARAKANI

 

Dodoma, 28 Mei 2025 — Mahakama Kuu ya Tanzania (Main Registry – Dodoma), leo imetoa hukumu ya kihistoria katika Shauri la Madai Na. 18/2023 (Judicial Review), lililofunguliwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Ndugu James Francis Mbatia, dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa chama hicho.
Katika hukumu iliyosomwa na Jaji A. Kagomba, Mahakama imetengua maamuzi yote ya Mkutano Mkuu wa NCCR-Mageuzi uliofanyika tarehe 24 Septemba 2022, uliomuondoa Mbatia kwenye nafasi ya Uenyekiti wa chama na kumfukuza uanachama.
Mbatia Alikuwa Mwanachama Halali
Akizungumza kuhusu hoja ya msingi iliyowasilishwa na upande wa wadaiwa kuwa Mbatia hakuwa mwanachama halali kwa kuwa kadi yake ilitolewa mwaka 1992 kabla ya chama kusajiliwa rasmi mwaka 1993, Jaji Kagomba amesema:
"Hoja hiyo haina mantiki yoyote kwa sababu mwaka 1992 ulikuwa ni mwaka wa usajili wa muda wa vyama vya siasa, na wanachama hao ndio waliowezesha chama kupata usajili wa kudumu. Hata Katiba ya NCCR-Mageuzi ni ya mwaka 1992."
Haki ya Kusikilizwa Yavunjwa
Kuhusu utaratibu wa Mkutano Mkuu uliofanyika Septemba 2022, Mahakama ilibaini kuwa Mbatia hakupata haki ya kisheria ya kusikilizwa kabla ya kuondolewa uanachama na uongozi wa chama.
"Mkutano huo ulikiuka misingi ya haki ya asili (natural justice), Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katiba ya NCCR-Mageuzi na Sheria za Vyama vya Siasa," alisisitiza Jaji Kagomba.
Maamuzi Yabatilishwa, Gharama Kulipwa
Kwa mujibu wa hukumu hiyo, Mahakama imetengua maamuzi yote yaliyotokana na mkutano huo, ikiwemo kumvua Mbatia nafasi ya uenyekiti na uanachama. Aidha, Mahakama imeamuru kuwa wadaiwa walipe gharama zote za kesi hiyo.
Kwa upande mwingine, bado haijafahamika kama upande wa wadaiwa utakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo, lakini kwa sasa, James Francis Mbatia amerejeshwa rasmi kama mwanachama na Mwenyekiti halali wa NCCR-Mageuzi.

0 Comments:

Post a Comment