Bunge la Ulaya Kufanya Mjadala wa Dharura Kuhusu Kesi ya Lissu

 


Bunge la Ulaya limepanga kufanya mjadala wa dharura Mei 7,  2025 kuhusu kesi ya Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambaye ni mmoja wa wapinzani wakuu wa kisiasa nchini Tanzania.


Kwa mujibu wa ratiba iliyochapishwa kwenye tovuti rasmi ya Bunge la Ulaya, mjadala huo unatarajiwa kuanza saa 7 mchana hadi saa 4 usiku kwa saa za Ulaya, na utagusia kwa kina masuala yanayohusiana na haki za binadamu, demokrasia na ukandamizaji wa kisiasa nchini Tanzania.


Tundu Lissu alikamatwa mwezi Aprili 2025, ikiwa ni miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu. 


Kukamatwa kwake kumezua taharuki ndani na nje ya nchi, huku wakosoaji wa serikali wakieleza kuwa ni sehemu ya mkakati wa kuzima sauti za upinzani kuelekea uchaguzi.


Chama chake, CHADEMA, kimetoa wito wa kufanyika kwa mageuzi ya mfumo wa uchaguzi, ikiwemo kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi, ili kuhakikisha uchaguzi wa haki, huru na wa kuaminika.


Baada ya mjadala huo, Bunge la Ulaya litaandaa azimio maalum lenye namba rejea 2025/2690 (RSP), ambalo litajadiliwa na kupigiwa kura na wabunge wa Ulaya siku inayofuata, Mei 8, 2025


Azimio hilo linaweza kuwa na athari kubwa kisiasa na kidiplomasia kwa uhusiano wa Umoja wa Ulaya na Tanzania.




0 Comments:

Post a Comment